Tanzania yapaa kimataifa katika kutoa huduma za matibabu ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi hiyo katika hafla fupi ya kuwapongeza madaktari bingwa wa moyo waliokwenda kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpongeza Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi hiyo Dkt. Angela Muhozya pamoja na timu ya wataalamu wa Taasisi hiyo waliokwenda nchini Malawi katika Hospitali ya Queen Elizabeth kwaajili ya kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza katika hafla fupi ya kuwapongeza madaktari bingwa wa moyo waliokwenda kutoa huduma za upimaji na matibabu katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.
******************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itaendelea kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa nchi zinazoizunguka Tanzania ili huduma hiyo iweze kuwafikia watu wengi zaidi na kuokoa maisha yao.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo
Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza madaktari bingwa wa moyo waliokwenda kutoa
huduma za upimaji na matibabu katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini
Malawi.
Dkt. Kisenge alisema Taasisi hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa
kutoka nchi za Afrika ya Mashariki na Kati ikiwemo Malawi lakini kutokana na
uhitaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nchini humu wakaona ni vyema waratibu
kambi ya upimaji na matibabu ya moyo na kuwatuma wataalamu wa JKCI kwenda kutoa
huduma kwa wananchi wa Malawi.
“Kwa namna ya kipekee ninamshukuru aliyekuwa Balozi wa Malawi
Mhe. Humphrey Polepole ambaye alitufuata na kutuomba tukatoe huduma za matibabu
ya kibingwa nchini humo kwani kuna uhitaji mkubwa wa huduma hiyo na aliichagua
Taasisi yetu kwa kuwa inatoa huduma bora za matibabu ya moyo hapa nchini na
katika nchi za Afrika Mashariki na Kati”.
“Baada ya wataalamu wa Taasisi yetu kwenda kutoa huduma
nchini Malawi imeonekana kuna wagonjwa wengi wanaohitaji kupata huduma za
kibingwa za matibabu ya moyo kwani huduma hizo hazipatikani nchini humo hivyo
basi ni nafasi kwa Tanzania kwenda kutoa huduma nchini Malawi na katika nchi za jirani ambazo hazina huduma za kibingwa za
matibabu ya moyo”.
“Wagonjwa hawa baada ya kufanyiwa uchunguzi wamepewa rufaa ya
kuja kutibiwa katika Taasisi yetu ambako ni karibu na Malawi ukilinganisha na
nchi zingine. Kwa kuja kwao hapa nchini nchi yetu itaongeza mapato pia tutakuwa
tumeutangaza utalii wa matibabu ambao ni maelekezo na maono ya Mhe. Samia
Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa nchi yetu iwe ni mahali ambapo watu watatoka katika nchi mbalimbali na kuja kupata huduma za matibabu”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye alikuwa
mkuu wa msafara wa wataalamu waliokwenda kutoa huduma nchini Malawi Dkt. Angela
Muhozya alisema wagonjwa waliowaona walikuwa wanahitaji huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
Dkt. Angela alisema wakiwa nchini Malawi walitoa huduma za
matibabu kwa watoto na watu wazima ambapo wengi wa wagonjwa walikuwa na matatizo ya shinikizo la juu la
damu, matundu, valvu za moyo na mishipa ya damu ya moyo kushindwa kupitisha
damu vizuri.
“Tulifanya upimaji kwa wagonjwa 724 kati ya hawa waliokuwa na
matatizo ya moyo ni 537. Waliohitaji rufaa walikuwa 201 kati yao 132 watafanyiwa
upasuaji wa moyo watoto wakiwa 78 na watu wazima 54 na waliohitaji kufanyiwa
uchunguzi na upasuaji kwa njia ya tundo dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab walikuwa
69 kati ya hao watoto 36 na watu wazima 33”.
“Wagonjwa 15 tuliwapa rufaa ya haraka kwaajili ya kufanyiwa upasuaji mkubwa au mdogo wa moyo”,
alisema Dkt. Angela.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Stella
Mongela alisema watoto wengi waliowaona walikuwa na matatizo ya moyo ya
kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika
mpangilio wake na wengine walikuwa na magonjwa ya moyo ya kuambukiza ambayo ni
Valvu za moyo kushindwa kufanya kazi vizuri.
“Watoto wengi walikuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo
ambayo hata watoto wa hapa nyumbani wanayo, tofauti iliyopo ni hapa nchini
huduma za matibabu ya kibingwa zinapatikana lakini kule huduma hizo hakuna na
hivyo wagonjwa kushindwa kupata huduma kwa wakati”, alisema Dkt. Stella.
Dkt. Stella aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa na
taasisi ya moyo yenye vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wa kutosha kwa kuwa na
huduma hiyo kunawasaidia watanzania wakiwemo watoto kupata huduma za matibabu
ya kibingwa kwa wakati.
Comments
Post a Comment