Malawi yaishukuru Tanzania kwa kutoa huduma za matibabu ya moyo
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Parvina Kazaura na mwenzake kutoka Hospitali ya Queen
Elizabeth iliyopo nchini Malawi wakiangalia majibu ya mgonjwa aliyefanya kipimo
cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram - Echo) wakati wa
kambi maalum ya siku tano iliyofanywa na madaktari hao nchini Malawi katika
Hospitali ya Queen Elizabeth
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Georgy Longopa na mwenzake bingwa wa magonjwa ya moyo
kutoka Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi Dkt. David McCalthy
wakijadili matibabu anayopaswa kupewa mgonjwa mara baada ya kumfanyia uchunguzi
wakati wa kambi maalum ya siku tano iliyofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa
kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi
Na: Mwandishi Maalum – Blantyre Malawi
**************************************************************************************************************************************
Serikali ya Malawi yaishukuru Serikali ya Tanzania
kwa kuwapeleka wataalam wa moyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi na matibabu ya
magonjwa ya moyo kwa wananchi wa nchi hiyo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya nchini Malawi Mhe. Khumbize
Chiponda alipotembelea Hospitali ya Queen Elizabeth kuangalia huduma zilizokuwa
zikitolewa na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati
wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo.
Mhe. Khumbize alisema Malawi na Tanzania wamekubaliana kuwa na
kushirikiano katika kujengeana uwezo kwani nchi hiyo bado haijaweza kuanzisha
hospitali ya moyo hivyo kupitia kambi hiyo wataenda kujitathimini uwezo wao
kama wanaweza kuanzisha kituo ambacho kitakuwa kinatoa huduma za matibabu ya
kibingwa ya moyo nchini humo.
“Ndugu zetu watanzania wapo mbele yetu katika kutoa huduma za
uchunguzi na matibabu ya moyo kwasababu yatari wameshafungua Taasisi ambayo
inatoa huduma za moyo na imewekeza wataalamu na vifaa vya kutosha, naamini
tukiendelea kupata ujuzi kama huu nasi tutaweza kufungua Hospitali ya Moyo”,
alisema Mhe. Khumbize
Mhe. Khumbize alisema matibabu ya moyo ni ya gharama, hadi
sasa Malawi ina wagonjwa zaidi ya mia tano wenye gamonjwa mbalimbali ya moyo wanaosubiria
kuwapeleka nje ya Malawi kwa ajili ya matibabu.
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Parvina Kazaura alisema
katika kambi hiyo walifanya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watu wazima na
watoto ambapo kila siku watoto zaidi ya 80 wamekuwa wakifanyiwa uchunguzi wa moyo
na kubaini watoto wengi walikuwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo na
wachache kuwa na magonjwa ya moyo waliyoyapata wakati wa ukuaji.
“Kwa bahati mbaya watoto wengi wenye magonjwa ya moyo ya
kuzaliwa nayo wamekuja wakiwa na umri mkubwa ambapo ilipaswa kufanyiwa upasuaji
mapema baada ya kuzaliwa lakini hawakufanyiwa kutokana na huduma hizi kutokuwepo
hapa Malawi”,
Dkt. Parvina alisema watoto ambao kutokana na umri wao kupita
wakati wa kufanyiwa upasuaji wa moyo wameangalia matibabu wanayoendelea
kuyapata na kuwashauri wataalam wa afya wanaowahudumia ni dawa gani wanapaswa
kuzitumia ili waweze kuwa sawa.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya magonjwa ya ndani kutoka
Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo Nchini Malawi Dkt. Chimota Phiri alisema kambi
ya matibabu ya moyo iliyofanywa na wenzeo kutoka JKCI imewapa mwanga wa
kuyatambua magonjwa mbalimbali ya moyo waliyonayo wananchi wa Malawi
“Nchi yetu sasa inatakiwa kuwekeza katika taaluma ya kibingwa
ya matibabu ya moyo ili wataalam wetu waweze kwenda kujifunza na kuwasaidia
wananchi wetu kupata huduma hapa nchini badala ya kuanza kuhangaika kutafuta
huduma za matibabu ya moyo nchi za mbali”, alisema Chimota
Lay Pastor Kachoka mwananchi wa Malawi aliyepatiwa huduma
katika kambi hiyo amewashukuru madaktari kutoka JKCI kwa kumfanyia uchunguzi wa
kina na kumshauri kuhudhuria kliniki ya matibabu ya moyo kila baada ya miezi
sita.
“Sisi wananchi wa Malawi tunahitaji sana huduma hizi kuwepo
hapa nchini kwetu, nawashauri wakati mwingine watakapoandaa kambi kama hii
waweke maeneo tofauti tofauti ya nchi yetu ili wananchi wote waweze kufaidika
na huduma hizi”, alisema Lay Postor
Comments
Post a Comment