Wananchi wa Manyara wapimwa moyo
Fundi sanifu wa moyo (Cardiovascular technologist ) wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Paschal Kondi akimpima kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mkazi wa Manyara wakati wa kambi maalum
ya siku tano inayofanywa na wataalam wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa
Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH)
Wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na
wenzao wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) wakiwapima wananchi shinikizo
la damu, sukari mwilini na mzunguko wa tumbo wakati wa kambi maalum ya siku
tano inayofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa
MRRH.
Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Manyara wakiwa katika foleni ya
kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya siku
tano inayofanywa na wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara
Na: JKCI
*******************************************************************************************************
Wananchi wa Mkoa wa Manyara wameishukuru Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwapeleka wataalam wa afya mabingwa wa moyo kwa
ajili ya kuwafanyia uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Hayo yamesemwa na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika
Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH)
kwa ajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano iliyoanza leo
ikifanywa na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao wa MRRH.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkazi wa Babati vijijini
Andrea Tluway alisema ujio wa mabingwa kutoka JKCI kwake imekuwa fursa ya
kuchunguza moyo wake kwani hakuwahi kupimwa moyo na amekuwa akisumbuliwa na
tatizo la shinikizo la damu.
“Niliposikia matangazo ya kambi hii sikupuuzia hii nafasi,
tofauti na kuwa na shida ya shinikizo la damu pia nimekuwa nikiona dalili
tofauti tofauti katika mwili wangu kama mapigo ya moyo kupiga kwa haraka,
maumivu makali upande wa kushoto wa kifua na moyo kuuma hivyo nikaona nivizuri
leo nikapima moyo wangu kufahamu kama nina shida ya moyo”, alisema Andrea
Aidha Andrea amewashauri wananchi wa mkoa wa Manyara na mikoa
ya jirani ambao bado hawajafika katika Hospitali hiyo kutumia nafasi hiyo
yakipekee ambayo Serikali ya awamu ya sita imewapa wananchi wa Manyara kufikiwa
na huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Agnes Hamad mkazi wa Manyara alisema miaka mitatu iliyopita
alivimba sehemu mbalimbali za mwili wake ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi
ilionekana kuwa upande mmoja wa moyo umejaa maji na kupatiwa dawa ambazo baada
ya kuzitumia na kurudi Hospitali aliona nafuu tofauti na alivyokuwa mwanzo.
Agnes anasema baada ya kusikia ujio wa Madaktari bingwa wa
moyo wa JKCI akaone ni wakati sasa kufanyiwa vipimo vya moyo na mabingwa hao
ili aweze kupata uhakika zaidi kama tatizo alilokuwa nalo mwanzo limeisha au
anahitaji matibabu zaidi.
“Naishukuru sana Serikali yetu kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete kutuletea wataalam karibu ili tuweze kutumia gharama kidogo kuchunguza
afya zetu tofauti na kama tungezifuata Dar es Salaam”, alisema Agnes
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Johnstone Kayandabila alisema JKCI
imeweka utaratibu wa kuwafuata wananchi mahali walipo kusogeza huduma karibu na
wananchi kuwasaidia wale ambao wasingeweza kupata nafasi ya kufuata huduma hizo
JKCI kupata huduma.
Dkt. Johnstone alisema wakazi wa Manyara wamejitokeza kwa
wingi na tayari siku ya kwanza wameshakutana na wagonjwa ambao wanahitaji
kupewa rufaa kwenda JKCI kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Kwa siku ya leo hadi mchana huu tumeshawapa rufaa watu
wazima wawili mmoja akiwa na maumivu ya kifua na mwingine mfumo wake wa umeme
wa moyo kuwa na hitilafu, pia watoto wawili ambao wana matundu kwenye moyo
tumewapa rufaa waweze kufika JKCI kwa
ajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo”, alisema Dkt. Johnstone
Naye kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara
(MRRH) Dkt. Yesiga Mutajwaa alisema Hospitali hiyo inatamani kuwe na muendelezo
wa ushirikiano baina ya JKCI na MRRH kwani MRRH bado ina changamoto katika
ufanyaji wa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram –
Echo)
Dkt. Yesiga alisema kupitia kambi hiyo wanaenda kuboresha
mashirikiano kwani MRRH ikipata wagonjwa hasa wale wanaohitaji upasuaji wa
moyo huwa hawana maamuzi nao zaidi ya
kuwapa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.
“Kwa wiki hii moja naamini wataalam wetu watapata nafasi ya
kujifunza lakini pia itatusaidia kufanya maamuzi kama tutawaomba JKCI warudi
tena kwa ajli ya kutufundisha au sisi tupeleke wataalam wetu JKCI kupata
uzoefu”, alisema Dkt. Yesiga
Comments
Post a Comment