Wataalam
wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao
kutoka mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid lenye makao yake
makuu mjini London nchini Uingereza wakifanya upasuaji wa kurekebisha mishipa
ya damu ya moyo wa mtoto wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upasuaji wa
moyo iliyomalizika leo katika Taasisi hiyo.
Wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu mjini London nchini Uingereza wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kambi maalum ya siku tano ya upasuaji wa moyo iliyofanyika JKCI.
*************************************************************************************************************************************************************************************
Watoto
427 wenye matatizo ya matundu kwenye moyo, matatizo ya mishipa ya damu na
Valve za moyo wamefanyiwa uchunguzi na
upasuaji katika kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto iliyomalizika leo
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Upasuaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kambi hiyo ya
siku tano ya upasuaji wa moyo kwa watoto ilianza tarehe 12/05/2023.
Dkt. Angela
alisema kambi ya upasuaji wa moyo
ilifanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo ya watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa
Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu mjini London nchini
Uingereza.
Alisema wataalam
hao kutoka Shirika la Muntada Aid walikuja nchini na vifaa vyao vilivyotumika
katika upasuaji huo wa watoto vyenye
thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500.
“Watoto 427
wamefanyiwa uchunguzi wa moyo ambapo kati yao watoto 41 wamefanyiwa upasuaji
kwa njia ya tundu dogo ambao unafanyika kwa kutumia mtambo wa Cathlab na watoto
18 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua”.
“Watoto waliofanyiwa
upasuaji wanaendelea vizuri kuna ambao wamesharuhusiwa kurudi nyumbani na
wengine wametoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kwenda wodini
kuendelea na matibabu ya dawa na mazoezi”, alisema Dkt.Angela.
Kwa upande
wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Delila Kimambo aliwashukuru wataalam wa JKCI na wenzao wa Shirika la Muntada Aid kupitia mradi wa Little Heart ambao wamefanikisha upasuaji
wa watoto waliokuwa wanasumbuliwa na magonjwa ya moyo.
“Ninalishukuru
Shirika la Muntada Aid kupitia mradi wao wa Little Heart ambao wamefanikisha
kambi hii ya uchunguzi na upasuaji wa moyo kwa watoto 427, JKCI imejifunza vitu
vingi kutoka kwenu na ninaamini mtarudi tena mwezi wa kumi na moja mwaka huu
kwaajili ya kuwahudumia watoto wa kitanzania wenye matatizo ya moyo”, alisema
Dkt. Delila.
Naye Meneja mradi
wa Shirika la Muntada Aid Kabir Miah alisema shirika hilo limekuwa likitoa huduma
mbalimbali zikiwemo za afya, elimu na misaada ya kibinadamu katika nchi 22 na hadi
sasa zaidi ya watu 262,000 wamenufaika na huduma hizo.
“Shirika la Muntada
Aid kupitia mradi wa Little Heart
limekuwa likifanya kambi maalum za matibabu ya kutoa huduma za upasuaji wa moyo
kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambapo kwa wakati mmoja tunatoa
huduma hii kwa watoto 50 hadi 60 lakini katika maeneo mengine idadi inaweza
kuongezeka”.
“Tunawataalam
wa afya katika nchi mbalimbali ambao wanashirikiana na wataalam wa Hospitali
tunayokwenda kutoa huduma ya upasuaji. Licha ya kufanya upasuaji wataalam wetu pia
wanatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wenzao wanaofanya nao kazi ili nao waweze
kutoa huduma kama zao”, alisema Kabir.
Nao wazazi
ambao watoto wao walitibiwa katika kambi hiyo waliishukuru Serikali kwa kujenga
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kusomesha wataalam na kununua vifaa tiba
vya kisasa ambavyo vimewasaidia watoto wao kupata huduma ya upasuaji hapa
nchini.
Diana Kulwa
kutoka mkoa wa Mwanza alisema mtoto wake
alikuwa na tatizo la tundu kwenye moyo na aligundua kuwa na tatizo hilo akiwa
na umri wa miaka mitatu na baadaye alipata rufaa kutoka hospitali ya Bugando na
kupelekwa JKCI kwaajili ya kupata matibabu ya kibingwa.
“Ninashukuru
sana kwa huduma niliyoipata kwani sikuwa na fedha za kulipia matibabu ya
mwanangu lakini nimepata msamaha wa matibabu na mwanangu kafanyiwa upasuaji na
anaendelea vizuri”.
“Niliambiwa
gharama za matibabu ni milioni nane na laki tano kwa kuwa sina uwezo
nimechangia shilingi laki tano na mwanangu kafanyiwa upasuaji. Ninaishukuru
sana Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kunihurumia na kumtibu mwanangu”,
alishukuru Diana.
Shija Matunda
aliwaomba kinamama wenye watoto walio na matatizo ya moyo wasiogope na kukata tamaa
kwani huduma za upasuaji zinapatikana hapa nchini hata kama mtu hana uwezo wa
kulipia anapata huduma kwani ukifika hospitali utaelekezwa utaratibu wa
kufuata.
“Ninawaomba
kina mama wenzangu kuwaleta watoto wao katika matibabu mwanangu alikuwa
anapumua haraka haraka baada ya kufanyiwa uchunguzi alikutwa na tundu kwenye moyo, amefanyiwa
upasuaji anaendelea vizuri”, alisema Shija.
Comments
Post a Comment