Wagonjwa 310 kutoka nje ya nchi watibiwa JKCI kwa kipindi cha miaka miwili
Mratibu wa matibabu nje ya nchi kutoka Wizara ya Afya Dkt.
Asha Mahita akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Peter Kisenge kitabu chanye mpango mkakati wa utalii tiba
kilichoandaliwa na kamati ya kitaifa ya utalii tiba leo wakati wa uzinduzi wa
kamati za utalii tiba kutoka Hospitali za Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya
Mifupa Muhimbili (MOI)na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) uliofanyika
katika Hoteli ya Hyatt Regency iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati za utalii tiba
kutoka Hospitali za Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI), Hospitali ya Mifupa Muhimbili (MOI), na Taasisi ya Saratani Ocean Road
(ORCI) uliofanyika leo katika Hoteli ya Hyatt Regency iliyopo jijini Dar es
Salaam.
Wagonjwa 310 kutoka nchi za Somalia,
Malawi, Kenya, Rwanda, Visiwa vya Comoro, Ethiopia, Burundi, Armenia, Norway na
Uingereza wamepata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo katika Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati za utalii tiba
zilizopo katika Hospitali za kibingwa hapa nchini Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema wagonjwa hao
wamepata matibabu hayo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo alisema JKCI katika
kuhamasisha utalii tiba mwaka jana imeshiriki maonyesho ya huduma inazozitoa
katika visiwa vya Como, wiki hii wataalamu wa Taasisi hiyo wako nchini Malawi
kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi
na matibabu ya moyo na baadaye inatarajia kwenda nchini Burundi na Jamhuri ya
watu wa Congo kutoa huduma hizo.
Dkt. Kisenge alisema katika Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka
mitatu kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaotoka nje ya Tanzania, kwa
mwaka 2022 waliona wagonjwa zaidi ya 200 na mwaka huu wa 2023 hadi sasa wametoa
huduma kwa wagonjwa 110.
“JKCI imetengeneza mpango mkakati ambao unafuata malengo
yaliyowekwa na kamati ya kitaifa ya utalii tiba kuhakikisha kwamba kupitia
sekta ya afya utalii unaongezeka hapa nchini”,.
“Ninaipongeza kamati ya kitaifa ya utalii tiba kwa kuwa
chachu ya kufanikisha malengo ya Rais wa Serikali ya awamu ya sita Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan ninaahidi Taasisi
yetu imejipanga kutangaza utalii tiba kwa vitendo”, alisema Dkt.Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge
amesema kuwa JKCI inatarajia kufanya mkutano mkubwa mwaka 2024 utakaoonyesha
nini kinafanywa na Taasisi hiyo na matarajio yao ni kuhakikisha kuwa zaidi ya
nchi 40 zinashiriki katika mkutano huo.
Akizungumza mara baada ya kuzindua kamati za utalii tiba Mratibu
wa matibabu nje ya nchi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Asha Mahita alisema hospitali
za kibingwa zinatakiwa kujenga uaminifu na ukarimu kwa wagonjwa wanaowahudumia ili
kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi kutibiwa kwani huduma zote
za kibingwa sasa hupatikana hapa nchini.
Dkt. Asha alisema dhana ya utalii tiba nchini ilikuwa bado haijaeleweka
vizuri hapo awali lakini tangu kuanza kwa kamati maalum ya utalii tiba
mabadiliko makubwa yametokea kwani sasa wagonjwa kutoka nchi nyingi za Afrika
wanakuja Tanzania kupata huduma za matibabu ya kibingwa yanayotolewa na
Hospitali zetu.
Dkt. Asha alisema lengo kubwa la utalii tiba ni pamoja na
kuongeza pato la nchi lakini pia mtu mmoja mmoja katika nchi kufaidika kupitia
utalii tiba kwani wagonjwa wanaofika watahitaji malazi na huduma nyingine hivyo
wote kwa pamoja kukuza uchumi wa nchi na uchumi binafsi.
“Kuzindua kamati za utalii tiba ni tukio kubwa katika sekta
ya tiba utalii hapa nchini, nawapongeza kwa niaba ya Wizara kwa kazi kubwa
ambayo kamati ya kitaifa ya utalii tiba imefanya tangu walipoteuliwa mwaka 2021
hadi sasa”, alisema Dkt. Asha
Aidha Dkt. Asha amezitaka Hospitali zote nchini kujitathmini
na kuamua zinataka kufanya nini ili kuendana na malengo ya wizara inapojiandaa
kutengeneza muongozo ambao utaleta majukumu ya kada zilizopo katika Hospitali
kuwezesha kila mfanyakazi kuchukua nafasi yake na kutekeleza majukumu yake.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya utalii tiba Prof.
Mohamed Janabi alisema kupitia kamati ya kitaifa ya utalii tiba wameweza
kuujulisha umma nini maana ya utalii tiba hivyo kupunguza idadi ya watu
waliokuwa wanakwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.
Prof. Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali
ya Taifa Muhimbili alisema kufikia mwaka 2030 Tanzania inatarajia kuwa na
watalii milioni tano waonafika hapa nchini kwa mwaka na kupitia watalii hao
wapo baadhi ambao watahitaji huduma za matibabu hivyo ni vyema Hospitali
zikaendelea kuboresha huduma na
kuvitunza vizuri vifaa tiba kwani ni vya gharama.
“Dhumuni letu kubwa kama kamati tunataka tupate angalau
asilimia 10 ya wagonjwa wanaokwenda nchi za ulaya kwaajili ya matibabu kutibiwa
katika nchi yetu kwasababu sasa vifaa tunavyo na wataalam kwaajili ya kutoa
huduma za kibingwa wapo wakutosha”, alisema Prof. Janabi.
Comments
Post a Comment