JKCI yawafikia viongozi, yawafanyia uchunguzi wa afya wakati wa mkutano wa CEO Forum 2026
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Moris Budotela akimsomea majibu Meneja Uhusiano kwa Umma Hifadhi
ya Ngorongoro Hamisi Dambaya wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya
inayofanyika katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu
wa taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali (CEO Forum 2026) katika Kituo
cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) jijini Arusha.
Viongozi na watendaji wakuu wa
taasisi za umma nchini wanufaika na huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa
yasiyoambukiza zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi,
mashirika ya umma na wakala wa serikali (CEO Forum 2026).
Huduma hizo zinatolewa katika
kambi maalumu inaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) ambapo
washiriki wa kikao kazi hicho wanafanyiwa uchunguzi wa utendaji kazi wa moyo, vipimo
vya figo, wingi wa mafuta kwenye damu na wingi wa sukari kwenye damu sambamba
na kupewa elimu ya kujua namba zao.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hii Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI-ALMC) Farida
Abdallah alisema kambi huduma za uchunguzi wa afya kwa viongozi hao ni za
muhimu kwani wakiwa na afya bora wataweza kutekeleza majukumu yao kwa weledi na
kuleta maendeleo ya nchi.
“Tumepata fursa ya kuwahudumia
wenyeviti wa bodi, wakurugenzi wa taasisi, mashirika ya umma na mashirika ya
kiserikali nchini, viongozi hao wameendelea kufika katika kitengo cha uchunguzi
wa magonjwa ya moyo kwaajili ya kujua namba zao”, alisema Dkt. Farida.
Dkt. Farida alisema sambamba na
uchunguzi wa afya ya moyo wataalamu wa JKCI wameendelea kutoa elimu ya lishe
bora kwa viongozi hao ili waweze kufahamu viashiria vya magonjwa ya moyo na
namna ya kukabiliana na magonjwa hayo.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano
kwa Umma wa Hifadhi ya Ngorongoro Hamisi Dambaya alisema amefurahishwa na
huduma aliyoipata kutoka kwa wataalamu wa JKCI kwani uchunguzi aliofanyiwa
umemsaidia kupata taarifa sahihi kuhusu afya yake.
“Nimefanyiwa uchunguzi wa afya na
kuhudumiwa vizuri, kikubwa nimefanyiwa vipimo vya moyo na kupata elimu ya kutosha
kuhusu magonjwa hayo. Watanzania wana
kila sababu ya kufika katika Taasisi hii na kuchunguza afya zao”, alisema
Dambaya.
Kambi hiyo inaendelea kutoa
huduma za uchunguzi na elimu ya afya kwa washiriki wa mkutano wa CEO Forum 2026
ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kinga na
utambuzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza.
.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment