Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani akisalimiana na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Masuala Mtambuka kutoka Bunge la Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EALA) Mhe. Mary Mugyenyi wakati wa ziara ya kamati hiyo
ilipotembelea JKCI kwaajili ya kuangalia huduma na miundombinu ya JKCI katika
kuwahudumia wananchi wa Afrika Mashariki wenye changamoto za magonjwa ya moyo.
Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani akiwaelezea
huduma zinazotolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi na dharura (ICU) wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Masuala Mtambuka kutoka Bunge la Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EALA) walipotembelea Taasisi hiyo kwaajili ya kuangalia huduma na
miundombinu ya JKCI katika kuwahudumia wananchi wa Afrika Mashariki wenye
changamoto za magonjwa ya moyo.
Wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Masuala Mtambuka kutoka Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wakiangalia
maabara ya kisasa inayotumia akili unde (AI) kuchakata sampuli walipotembelea
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kuangalia huduma na
miundombinu ya JKCI katika kuwahudumia wananchi wa Afrika Mashariki wenye
changamoto za magonjwa ya moyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Masuala Mtambuka kutoka Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA)
Mhe. Mary Mugyenyi akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kuangalia huduma na miundombinu JKCI katika
kuwahudumia wananchi wa Afrika Mashariki wenye changamoto za magonjwa ya moyo.
Picha Na
***********************************************************************************************************
Wabunge wa Kamati ya
Kudumu ya Masuala Mtambuka kutoka Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wapongeza
uwezo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kutoa huduma za kibingwa
na ubingwa bobezi katika matibabu ya moyo.
Pongezi hizo zimetolewa
na wabunge hao walipotembelea Taasisi hiyo kwaajili ya kuangalia miundombinu, uwekezaji
na uwezo wake katika kutoa huduma za matibabu, mafunzo na kutumia teknolojia za
kisasa katika kukabiliana na magonjwa ya moyo.
Akizungumza wakati wa
ziara hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Naizihijwa Majani alisema ziara ya wabunge hao imeonesha kujiridhisha kwao
kutokana na utayari wa JKCI katika kutekeleza majukumu yake kama Kituo cha
Umahiri Afrika Mashariki na Kati katika kutoa huduma bobezi za matibabu ya moyo
“Tutakapokamilisha ujenzi
wa JKCI mpya inayojengwa Mloganzila yenye vitanda 600 uwezo wetu wa kuhudumia
wananchi utakuwa mkubwa hivyo kutuwezesha kuhudumia hata wananchi wote kutoka
Africa Mashariki kwakua tutakuwa na miundombinu ya kutosha”, alisema Dkt. Naizihijwa
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Masuala Mtambuka kutoka Bunge la Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EALA) Mhe. Mary Mugyenyi alisema wabunge wa kamati yake wamevutiwa
na maendeleo yaliyofikiwa na JKCI katika kutoa huduma, mafunzo na matumizi ya
teknolojia za kisasa yanayofanyika katika matibabu ya magonjwa ya moyo.
“Wananchi wa Afrika
Mashariki wanapaswa kujua kwamba kwa sasa hawahitaji kwenda nchini India,
Uturuki na maeneo mengine kutafuta matibabu ya moyo kwani Taasisi hii ni muhimu
sana kwa Afrika Mashariki katika kutoa huduma hizo”, alisema Mhe. Mary.
Akielezea maendeleo
katika sekta ya afya Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Mhe.
Ansar Abubakary Kachwamba alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki imeweka mpango wa
kuanzisha vituo vya umahiri katika maeneo mbalimbali ambapo Tanzania imepewa
jukumu la kuwa kituo cha umahiri katika kutoa huduma bingwa bobezi za matibabu
ya moyo.
“Miaka kumi iliyopita
kupata matibabu ya moyo hata upasuaji mdogo tu ilikuwa lazima ulipe mamilioni
ya pesa ili uweze kwenda nchini India, Afrika Kusini au Uturuki kwa ajili ya
matibabu, sasa matibabu hayo yanafanyika hapa JKCI, haya ni mafanikio makubwa
kwa Tanzania na Afrika Mashariki”, alisema Mhe. Kachwamba.
Ziara ya Wabunge wa
Kamati ya Kudumu ya Masuala Mtambuka kutoka Bunge la Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EALA) imetoa fursa kwa wabunge hao kuona namna Tanzania
inavyotekeleza mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kuwa kituo cha umahiri katika
kutoa huduma bingwa bobezi za matibabu ya moyo.
-
Mwisho -
Comments
Post a Comment