JKCI yaweka msingi wa kuanza upandikizaji wa moyo nchini
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani akizungumza
wakati wa kikao cha utekelezaji wa mpango wa upandikizaji moyo kilichofanyika
leo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na wataalamu kutoka nchini Misri
na Kuwait.
Naibu Katibu Mkuu wa
Umoja wa Nchi za Kiarabu Mhe. Balozi Mohand Salah Ladjouzi akizungumza wakati
wa kikao cha utekelezaji wa mpango wa upandikizaji moyo unaotarajiwa kuanza
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wataalamu
kutoka nchini Misri na Kuwait.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba
kutoka Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea akizungumza wakati wa kikao cha
utekelezaji wa mpango wa upandikizaji moyo unaotarajiwa kuanza katika Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchini Misri
na Kuwait.
Baadhi ya wataalamu wa afya walioshiriki katika kikao cha utekelezaji wa mpango wa upandikizaji moyo unaotarajiwa kuanza katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchini Misri na Kuwait wakifuatilia mada zilizokuwa zikiendelea.
Picha Na JKCI
*******************************************************************************************************************
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka nchini Misri na Kuwait waanza maandalizi ya namna ya kutoa huduma za matibabu ya upandikizaji wa moyo nchini.
Hatua hiyo imelenga
kuangalia namna ambavyo wataalamu hao watafikia malengo ikiwemo kuwekeza katika
ujuzi wa wataalamu, kuandaa miongozo, na kuweka mazingira muhimu
yatakayowezesha huduma kuanza kutolewa hapa nchini.
Akizungumza wakati wa kikao
cha utekelezaji wa mpango wa upandikizaji moyo Mkurugenzi wa Huduma za Tiba
kutoka Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea alisema Serikali imeanza kutekeleza
mpango wa huduma ya upandikizaji wa moyo ikiwa ni sehemu ya jitihada za
kuongeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini katika kutekeleza Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2050.
“Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2050 imeelekeza ifikapo mwaka 2050 Tanzania iwe na uwezo wa
kutosheleza kutoa huduma za kibingwa bobezi ndani ya nchi, kwa sasa tayari
tunazo huduma nyingi kubwa hivyo tukaona ni wakati sasa kuanza taratibu za
kuwezesha huduma za upandikizaji wa moyo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hizo”,
alisema Dkt. Nyembea
Dkt Nyembea alisema
Tanzania imekuwa ikisafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi kupata matibabu ya
kupandikiza moyo ambapo gharama kwa mgonjwa mmoja ni kati ya shilingi milioni
200 hadi shilingi milioni 250 hivyo kama huduma hizo zitapatikana nchini
gharama zake zitapungua hadi kufikia nusu yake.
“Upandikizaji wa moyo
unahitaji utaalamu wa hali ya juu, vifaa vya kisasa pamoja na mazingira ya
kufanya upasuaji huo, hivyo tukaona ni vyema kuwa na ushirikiano wa ndani na
ushirikiano wa kimataifa kama ambavyo leo tumekutana na wataalamu hawa kutoka
nchini Misri na Kuwait ambao watashirikiana nasi hadi tutakapotimiza lengo la
kupandikiza moyo kwa wagonjwa waliopo nchini”, alisema Dkt. Nyembea
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa
Majani alisema kuanzishwa kwa mpango huo ni hatua muhimu katika safari ya JKCI
ya kupanua matibabu ya moyo na kuwafikia wagonjwa ambao kwa sasa wanakosa
huduma hizo nchini.
“Siku ya leo tunaanzisha
safari yetu ya mafanikio, kwa kipindi cha miaka 11 tumeendelea kukua na kuwa
Taasisi tegemezi Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania, safari hii itatufanya
tuendelee kutambulika, kusaidia wagonjwa na kutimiza malengo ya Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2050”, alisema Dkt. Naizihijwa
Dkt. Naizihijwa alisema JKCI
umeliona kundi moja la wagonjwa ambao bado hawajalifikia, kundi hilo ni la
wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi kabisa hivyo wakaona ni wakati
sasa wa kutatua changamoto za wagonjwa hao kwa kuanzisha huduma ya kupandikiza
moyo nchini.
“Huduma hii si ndogo,
tunapoelekea kuanza kutoa huduma ya upandikizaji wa moyo tunapaswa kuwa sehemu
ya kuwahudumia wagonjwa kutoka Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na Afrika
Magharibi kwani kwa sasa upande wa Afrika huduma hizi zinatolewa Afrika Kusini,
Misri na maeneo mengine machache”, alisema Dkt. Naizihijwa
Naye Naibu Katibu Mkuu wa
Umoja wa Nchi za Kiarabu Mhe. Balozi Mohand Salah Ladjouzi alisema ushirikiano
kati ya Tanzania na wadau wa nchi za Kiarabu umelenga kuwajenga uwezo wataalamu
kutoka nchini Tanzania kupitia mafunzo ya vitendo kuboresha ujuzi wa kitabibu.
“Kwa pamoja
hatutawasaidia tu wagonjwa wanaohitaji huduma za kupandikizwa moyo bali pia
kutoa mafunzo ya vitendo yatakayowawezesha wataalamu wa ndani kuendeleza ujuzi huo”,
alisema Mhe. Balozi Ladjouzi.
Hatua hiyo inaweka msingi
wa safari mpya ya JKCI kuelekea kuanzisha huduma ya upandikizaji wa moyo nchini
huku maandalizi yakilenga kuhakikisha wataalamu, vifaa, mifumo ya kisheria na
mazingira muhimu ya huduma vinakuwa tayari kabla ya kuanza kwa matibabu hayo.
-
Mwisho -
Comments
Post a Comment