“Tumieni maonesho ya madini kupima afya ya moyo” RMO Geita Dkt. Omari Sukari

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Omari Sukari akimsikiliza Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.  Moses Manumbu alipotembelea banda la Taasisi hiyo lililopo katika maonesho ya tisa ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili mjini Geita.


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Omari Sukari akisaini kitabu cha wageni  alipotembelea banda la JKCI lililopo katika maonesho ya tisa ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili mjini Geita.


 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Omari Sukari akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipotembelea banda la JKCI lililopo katika maonesho ya tisa ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili mjini Geita.

Picha na JKCI

******************************************************************************************************
Wananchi wa Mkoa wa Geita na maeneo jirani wametakiwa kutumia fursa adhimu ya maonesho ya tisa ya kitaifa ya teknolojia ya madini kufanya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza ili kuepuka gharama kubwa za matibabu zinazoweza kujitokeza badaye.

Rai hiyo imetolewa leo na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Omari Sukari alipotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) lililopo katika maonesho hayo na kuangalia muitikio wa wananchi katika kufanya uchunguzi wa afya.

Dkt. Sukari alisisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara kwani takwimu alizopewa katika banda la JKCI zimeonesha kuwa wananchi zaidi ya 400 wamejitokeza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo ambapo miongoni mwao zaidi ya watu 130 wamegundulika kuwa na shinikizo la juu la damu, zaidi ya 70 wamegundulika kuwa na ugonjwa wa moyo huku zaidi ya 20 wakigundulika kuwa na tatizo la kisukari.

 “Hii ni changamoto kwa mkoa wa Geita na maeneo jirani hivyo niwaombe wananchi wazingatie ushauri wa lishe kutoka kwa wataalamu na kuchukua hatua, hapo awali tulizoea kuwa magonjwa ya moyo huwapata zaidi watu wa mijini kutokana na mtindo wa maisha usiofaa, hivyo kwa idadi hii ni vema kuchukua hatua za haraka ili kujikinga”, alisema Dkt. Sukari.

Pamoja na mambo mengine Dkt. Sukari aliipongeza JKCI kwa kuendelea kutumia fursa za maonesho kusogeza huduma za kibingwa na bobezi za magonjwa ya moyo karibu na wananchi.

“Natoa pongezi kwa serikali na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI kwa kuendelea kuwajali wananchi waliopo pembezoni na kutuletea wataalamu ambao wanatoa elimu nzuri ya lishe ili kujikinga na magonjwa yasiyoyakuambukiza”, alisema Dkt. Sukari.

Mmoja wa wananchi waliofika katika banda la JKCI katika maonesho hayo Lule Joseph mkazi wa Geita vijijini alisema kupitia maonesho hayo amepata fursa ya kufanyiwa vipimo, kupata elimu na ushauri kuhusu afya yake bila gharama.

“Mbali na kufanyiwa uchunguzi wa afya bure pia nimepewa ushauri bure, naomba JKCI iendelee kushiriki katika maonesho haya ili wananchi ambao hatuna uwezo tuweze kupata huduma hizi za kibingwa”, alisema Lule



Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma