Magonjwa ya moyo husababisha vifo vya watu milioni 20 duniani kila mwaka

Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Engerasiya Kifai na Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi JKCI Robert Mallya wakimpatia zawadi mgonjwa aliyelazwa katika wodi za wagonjwa maalumu (VIP) wakati wa kuadhimisha siku ya moyo duniani ambayo uadhimishwa kila ifikapo tarehe 29 mwezi Septemba.

Afisa Huduma kwa Wateja wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Abubakari Mussa akimpatia zawadi mgonjwa anayetibiwa katika Taasisi hiyo tawi la Oyster bay wakati wa kuadhimisha siku ya moyo duniani ambayo uadhimishwa kila ifikapo tarehe 29 mwezi Septemba.

Mfamasia wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Martha Msechu akimpatia zawadi mgonjwa anayetibiwa katika Taasisi hiyo tawi la Kariakoo wakati wa kuadhimisha siku ya moyo duniani ambayo uadhimishwa kila ifikapo tarehe 29 mwezi Septemba.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyofanyika leo katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe jijini Dar es Salaam.

Afisa lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingindo akimpatia elimu ya lishe bora mwananchi aliyejitokeza kufanya uchunguzi wa afya wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyokuwa yakifanyika katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe leo jijini Dar es Salaam.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Silvia Milanzi akimpima joto la mwili mwananchi aliyejitokeza kufanya uchunguzi wa afya wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyokuwa yakifanyika leo katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe jijini Dar es Salaam.

Na JKCI

*****************************************************************************************************

Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu yanaendelea kuwa miongoni mwa changamoto kubwa za kiafya, huku yakisababisha vifo takribani kwa watu milioni 20 duniani kila mwaka.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani alisema ukubwa wa tatizo la magonjwa ya moyo unahitaji jamii kuwa makini na afya ya moyo na kuchukua hatua mapema.

Dkt. Naizihijwa alisema dalili mbalimbali za magonjwa ya moyo ikiwemo kuishiwa pumzi, maumivu ya kifua, kuvimba miguu, mapigo ya moyo kwenda mbio na uchovu zinaweza kujitokeza baada ya moyo kuwa umeathirika kwa muda mrefu.

“Kauli mbiu ya mwaka huu inatukumbusha umuhimu wa kuusikiliza moyo wetu kwa makini, kwa sababu ugonjwa wa moyo unaweza kuanza bila dalili na pale dalili zinapoanza kujitokeza wakati mwingine huwa ni ishara kwamba moyo umeathirika kwa muda mrefu”, alisema Dkt. Naizihijwa

Dkt. Naizihijwa alisema mara nyingi jamii hupuuza dalili zinazohusishwa na magonjwa ya moyo na kusubiri hadi hali inapokuwa mbaya jambo linaloweza kuathiri afya ya mgonjwa zaidi.

“Ujumbe wetu leo ni kwamba, sikiliza moyo wako kwa makini na chukua hatua mapema. Jamii isisubiri hadi dalili ziwe kubwa ndipo itafute huduma za afya”, alisema Dkt. Naizihijwa

Akizungumzia hali ya magonjwa hayo nchini Tanzania, Dkt. Naizihijwa alisema kumekuwa na ongezeko la tatizo la shinikizo la juu la damu ambalo limekuwa miongoni mwa vihatarishi vikubwa vya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

“Takwimu zinaonesha kuwa mtu mmoja kati ya watu wazima wanne ana tatizo la shinikizo la juu la damu, hali inayodhihirisha umuhimu wa jamii kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuzingatia mtindo bora wa maisha”, alisema Dkt. Naizihijwa

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Engerasiya Kifai aliihasa jamii kujua namba zao za afya kupitia kampeni inayofanywa na Wizara ya Afya pamoja na Taasisi hiyo kwani kuna umuhimu wa kila mwananchi kujua namba zake.

Dkt. Kifai alisema jamii inapoweza kutambua mapema mabadiliko yoyote katika moyo kunakuwa na urahisi wa kutibu na kuleta mafanikio mazuri tofauti na mabadiliko hayo yakichelewa kutibiwa.

“Tuwe wepesi wa kutambua mabadiliko yanayojitokeza katika miili yetu, tusiyachukulie mabadiliko hayo kama kitu cha kawaida kwasababu kuna dalili ambazo zimejificha sana hivyo siku zikijitokeza unakuwa umeshachelewa kutibu tatizo”, alisema Dkt. Kifai

Naye mwananchi aliyepata huduma wakati wa maadhimisho hayo Sakimembe Cosmas ameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuendelea kuijali jamii na kuwafanyia uchunguzi wa afya mara kwa mara ili wasiweze kukutana na changamoto za magonjwa ya moyo.

Sakimembe alisema watanzania wanapaswa kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya na kuacha kusikiliza watu ambao wamekuwa wakitoa ushauri bila ya kuwa na ujuzi katika fani za afya.

“Afya ni mtaji tusicheze na afya zetu, tunaposikia kuhusu huduma za kufanya uchunguzi wa afya tujitokeze na kupima kwani wataalamu wanatuambia dalili za magonjwa ya moyo wakati mwingine unaweza usizione”, alisema Sakimembe

Kauli mbiu ya mwaka huu “Usikose hata pigo moja la moyo” inatoa ujumbe muhimu kwa jamii wa kuusikiliza na kuutunza moyo kwa kuwa baadhi ya magonjwa ya moyo yanaweza kuanza bila kuonesha dalili za wazi.


 

 

Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma