CRDB Benki yachangia milioni 100 matibabu ya moyo kwa watoto
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Tulia Ackson akimkabidhi mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani hundi ya shilingi milioni 100
fedha iliyokusanywa kutoka kwa washiriki wa mbio za CRDB kwaajili ya kuchangia
matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika Viwanja
vya Farasi Oysterbay vilivyopo jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi hiyo mara baada ya kupokea hundi ya shilingi milioni 100 fedha zilizokusanywa kwa washiriki wa mbio za CRDB msimu wa sita kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI
Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) wakishiriki katika mazoezi ya viungo mara baada ya kumalizika kwa mbio
za CRDB zilizofanyika leo katika Viwanja vya Farasi Oysterbay vilivyopo jijini
Dar es Saalam kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo
wanaotibiwa JKCI.
Kaimu Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo akishiriki katika mbio za CRDB zilizofanyika leo katika viwanja vya Farasi Oysterbay vilivyopo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya na familia yake wakirikishi katika mbio za CRDB zilizofanyika leo katika viwanja vya Farasi Oysterbay vilivyopo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Na: JKCI
*******************************************************************************************************
Shilingi milioni 100 zimetolewa na Benki ya CRDB kupitia mbio
za CRDB msimu wa sita kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa
ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza wakati wa mbio hizo zilizofanyika leo katika
viwanja vya Farasi vilivyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson alisema mbio hizo
zimeyaunganisha mataifa 27 na kuwakutanisha washiriki zaidi ya elfu 16 ambao
kwa kukimbia kwao wameweza kuchangia matibabu ya watoto wanaohitaji upasuaji wa
moyo.
Mhe. Dkt. Tulia alisema CRDB Benki imeweza kusambaza tabasamu
kwa kipindi cha miaka mitano kwa kuhakikisha watoto zaidi ya 500 wenye magonjwa
ya moyo wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) na afya zao kurejea.
Aidha Mhe. Dkt. Tulia aliwashukuru wadau wa Benki ya CRDB kwa
kuungana na benki hiyo kukusanya fedha kwaajili ya matibabu ya watoto wenye
magonjwa ya moyo, wanawake wenye ujauzito hatarishi na vinajana wanaohitaji
kuinuliwa kiuchumi.
“Mchango unaotolewa na Benki ya CRDB katika sekta ya afya umemuwezesha
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupata tuzo inayotambua kasi kubwa iliyopo katika
kuboresha miundombinu ya afya, huduma za afya ikiwemo kushusha vifo vya mama na
mtoto ambayo imemuweka kwenye historia duniani”, alisema Mhe. Dkt. Tulia
Mhe. Dkt. Tulia alitoa wito kwa jamii kufanya mazoezi ili
iweze kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kuzingatia afya ya mwili
kulisaidia taifa kuwa na watu wenye afya bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji kutoka Benki ya CRDB Abdulmajid
Nsekela alisema mbio za CRDB msimu wa sita zinaenda sambamba na kusherehekea
miaka 30 ya benki hiyo huku akiainisha kuwa kwa kipindi chote hicho benki hiyo
imekuwa ikichukua asilimia 1 ya pato lake na kurudisha katika jamii kupitia
michezo, afya, elimu na mambo mengine.
“Katika mbio hizi za msimu wa sita tulijiwekea malengo ya
kupata bilioni 2 ambazo kwa hakika tumeweza kuzipata na hivyo tumeelekeza kiasi
cha Tshs. Milioni 100 katika Hospitali ya CCBRT kusaidia wanawake wenye
ujauzito hatarishi, Milioni 100 kwenda JKCI kusaidia matibabu ya watoto wenye
magonjwa ya moyo na Milioni 250 kwaajili ya programu mbalimbali za vijana”,
alisema Nsekela
Nsekela alisema misimu sita ya mbio za CRDB imekuwa
ikiwawezesha wadau wake wakuu watatu wakiwemo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Hospitali ya CCBRT na Vijana kupitia programu mbalimbali za maendeleo.
Comments
Post a Comment