Wasimamizi wa maeneo ya kazi JKCI watakiwa kuwa walezi bora kwa watumishi
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na Wasimamizi wa maeneo
mbalimbali ya kazi wa Taasisi hiyo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili
yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha
mkoani Pwani.
Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Abdulrahman Muya akizungumza na wasimamizi wa maeneo mbalimbali
ya kazi wa taasisi hiyo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uongozi yaliyofanyika
jana katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani
Pwani.
Baadhi ya wasimamizi wa maeneo mbalimbali ya kazi wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza mada zilizokuwa zikiendelea wakati
wa ufunguzi wa mafunzo ya uongozi uliofanyika jana katika Shule ya Uongozi ya
Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Picha na JKCI
************************************************************************************************************
Wasimamizi wa maeneo mbalimbali ya kazi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuwa walezi bora kwa watumishi wanaowaongoza
ili kuongeza mshikamano wa kikazi, kuimarisha utendaji na kuhakikisha huduma
bora zinatolewa kwa wagonjwa.
Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt.
Peter Kisenge, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wasimamizi
wa wa maeneo mbalimbali wa taasisi hiyo. Mafunzo hayo yanafanyika katika Shule
ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Dkt. Kisenge alisema wasimamizi wa vitengo hukutana na
changamoto mbalimbali za kikazi kutoka kwa watumishi wanaowasimamia, hivyo ni
muhimu wawe walezi na viongozi bora ili kuwasaidia watumishi kutatua changamoto
hizo na kufanikisha malengo ya taasisi.
“Mafunzo haya ya uongozi niliona myapate kwani nyie ni sehemu
ya viongozi wa taasisi yetu. Mkitoka hapa mkayafanyie kazi mtakayoelekezwa na
kuyatengenezea mikakati mizuri ili kuboresha huduma zetu”, alisema Dkt.
Kisenge.
Kwa upande wake Mkuu wa Utawala wa Shule ya Uongozi ya
Mwalimu Julius Nyerere Priscilla Mkini alisema mafunzo hayo yataleta mabadiliko
chanya katika utendaji kazi na kuimarisha mshirikiano kati ya wasimamizi na
watumishi wanaowaongoza.
“Siku hizi mbili mkizitumia ipasavyo mtaweza kutimiza lengo
lililowaleta hapa na kuwa viongozi bora kwa wengine”, alisema Mkini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali
Watu wa JKCI, Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu Abdulrahman Muya alisema mafunzo hayo yamelenga kuwaunganisha
wasimamizi wa vitengo ili kubadilishana uzoefu, kuimarisha mshirikiano na
kupata ujuzi wa namna bora ya kuongoza watumishi.
Muya aliongeza kuwa washiriki wa mafunzo hayo watajifunza
wajibu wao katika kusimamia rasilimali za umma, namna ya kutambua hisia za watu
wanaowaongoza, uadilifu na kujenga ushirikiano kazini.
“Idara ya Utawala na Rasilimali Watu itaendelea kutoa mafunzo
ya mara kwa mara kwa wafanyakazi ili kuimarisha utendaji. Ninaamini kwa pamoja
tutaweza kufikia malengo tuliyojiwekea”, alisema Muya.




Comments
Post a Comment