JKCI kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo mashindano ya CHAN


 Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph - ECHO) mchezaji wa mpira wa miguu.

Na: JKCI

***************************************************************************************************

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) itatoa huduma za  uchunguzi na matibabu ya  moyo bila malipo kwa wananchi watakaohudhuria katika mashindano ya kimataifa ya wachezaji wa ndani wa Africa (CHAN) yanayoanza  leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo jijini Dar es Salaam.
 
Upimaji huo unaofanywa na JKCI ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika michezo (Sports Cardiology Initiatives) unaolenga kutoa elimu, uchunguzi wa mapema na kuhamasisha jamii kuhusu afya ya moyo kwa wapenzi wa michezo na wanamichezo wenyewe.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda alisema kupitia michuano hiyo wanatoa nafasi kwa maelfu ya watanzania kujua hali ya  mioyo yao ili waweze kuchukua hatua mapema na kuepuka matatizo makubwa ya kiafya yanayoweza kuwapata baadaye.

“Afya ya moyo ni jambo la msingi kwa ustawi wa jamii, kwa kuzingatia hilo kupitia michuano hii tutawafanyia vipimo mbalimbali wananchi ikiwemo kipimo cha shinikizo la damu (BP), kipimo cha kuangalia kiwango cha sukari mwilini, kipimo cha kuangalia mapigo ya moyo, pamoja na elimu ya lishe na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa wa moyo”, alisema Dkt. Eva

Dkt. Eva alisema huduma hizo zinatolewa na wataalamu wa afya mabingwa na bobezi wa moyo kutoka JKCI katika kituo maalum kilichopo katika Uwanja wa Mkapa.

“Upimaji huu umelenga kuwafikia si tu mashabiki wa michezo, bali pia wanamichezo, maofisa wa timu na jamii kwa ujumla ikiwa ni hatua ya kuhakikisha wanamichezo na mashabiki wanakuwa na afya bora ya moyo hasa wakati huu ambapo magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka kwa kasi nchini na duniani kote”, alisema Dkt. Eva

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ilizindua programu ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo na mashabiki wa michezo nchini mapema mwezi Juni mwaka huu lengo likiwa ni kulinda afya za mioyo ya wanamichezo nchini.


Comments

Popular posts from this blog

Wateja wa CRDB kutibiwa JKCI kwa punguzo la asilimia 50%

Wanawake wa JKCI SACCOS wanaongoza kwa kumiliki hisa

JKCI kutanua huduma za matibabu ya moyo nchini