Rais wa Zambia aipongeza Tanzania kushiriki maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara

Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichilema akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule alipotembelea banda la Tanzania lililopo katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka. Tanzania inashiriki katika maonesho hayo kwa kutangaza huduma za matibabu ya ubingwa bobezi na huduma za usafirishaji zinazopatikana nchini.
Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule akimweleza Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichilema huduma za matibabu ya ubingwa bobezi na huduma za usafirishaji zinazopatikana nchini alipotembelea banda la Tanzania lililopo katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka.
Washiriki wa maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia kutoka Tanzania wakiwa katipa picha ya pamoja mara baada ya kufunguliwa kwa maonesho hayo yanayofanyika jijini Lusaka. Tanzania inashiriki katika maonesho hayo kwa kutangaza huduma za matibabu ya ubingwa bobezi na huduma za usafirishaji zinazopatikana nchini.
***********************************************************************************************************************************************************************************************
Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichilema ameipongeza Tanzania kwa kushiriki katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia ambayo yametumika kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa kiafya na usafirishaji baina ya nchi hizo mbili.
Pongezi hizo amezitoa leo jijini Lusaka alipotembelea banda
la Tanzania kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya ubingwa bobezi zinazopatikana
nchini pamoja na huduma za usafirishaji.
Mhe. Rais Hichilema alisema kushiriki
kwa Tanzania katika maonesho hayo ni ishara kuwa ushirikiano uliopo baina ya
nchi hizo mbili ni mkubwa na unalenga kuwasaidia wananchi.
“Ninashukuru kwa
ushirikiano ulipo baina ya Hospitali ya Moyo ya Zambia na Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI), kuwepo kwa ushirikiano huu wa kutibu wagonjwa na kutoa
mafunzo kwa wataalamu wa afya kunaokoa maisha ya watu wenye matataizo ya moyo”.
“Kupitia mitandao ya kijamii nimeona huduma za upasuaji wa
moyo zinazotolewa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI) nimevutiwa na huduma hizo ni nzuri nimeona
mashine za kisasa na wataalamu wa kutosha pia mazingira ya hospitali ni mazuri,
hongereni sana”, alisema Mhe. Rais Hichilema.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule alimshukuru
Mhe. Rais Hichilema kwa kutembelea banda hilo na kusema kuwa Tanzania
itaendelea kushiriki katika maonesho hayo kwa kuonesha huduma mbalimbali
zinazopatikana nchini humo.
“Katika banda hili kuna taasisi kubwa tano ambazo ni Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili
(MOI), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TPA) na Shirika la Ndege la Air Tanzania ambazo zinatoa huduma za
afya na usafirishaji”.
Tanzania imeshiriki katika maonesho hayo ikiwa na lengo la kutangaza huduma za matibabu ya kibingwa na huduma za usafirishaji zinazopatikana nchini kwa wananchi wa Zambia na mataifa mengine yanayoshiriki katika maonesho hayo.


Comments
Post a Comment