JKCI yaonyesha matumaini kwa wazazi wa watoto wenye shida ya moyo Sinyanga


Baadhi ya wazazi wakiwa na watoto wao wakisubiri kupata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo kwa watoto wakati wa kambi maalum ya siku tano ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH).
******************************************************************************************************************************
Changamoto ya kiuchumi kwa jamii imekuwa ni kikwazo kwa baadhi watoto kuendelea na matibabu ya moyo hali iliyosababisha kuchelewa kupata matibabu ambayo yangeokoa maisha yao.
Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa
watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nuru Letara wakati akizungumza
na waandishi wa habari katika kambi maalum ya matibabu ya moyo yanayofanyika katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH).
Dkt. Nuru alisema wazazi na walezi wengi wanakutana na
changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazopelekea kushindwa kuwapeleka watoto wao
hospitali kupata matibabu.
“Changamoto zipo nyingi ila changamoto kubwa ni hali duni ya uchumi
ambayo inasababisha wazazi na walezi kukosa nauli vilevile kukosa pesa ya
kulipia gharama za matibabu, lakini tunapokutana nao tunawatia moyo na
kuwasaodia”, alisema Dkt. Nuru.
Dkt. Nuru alisema miongoni mwa wagonjwa waliopewa rufaa katika
kambi hiyo ni mtoto aliyegendulika kuwa na tatizo la moyo kwenye kambi ya matibabu ya moyo iliyofanywa na wataalamu
wa JKCI mwaka mmoja uliopita lakini hakuweza kwenda kufanyiwa upasuaji kutokana na changamoto za kifedha.
“Katika kambi hii tumempa dawa za awali za kutumia pia
tumempa barua ya rufaa ya kuja kutibiwa JKCI. Kila kitu kikienda sawa
atafanyiwa upasuaji wa ,oyo mwanzoni mwa
mwezi Septemba mwaka huu katika kambi maalumu ya madaktari kutoka nchini Saudi
Arabia”, alisema Dkt. Nuru.
Dkt. Nuru pia aliwaomba wazazi kujua afya za watoto wao kwa kujua
dalili za magonjwa ya moyo ili waweze kupata matibabu mapema.
Kwa upande wake Bibi wa mtoto mwenye tatizo la moyo Monica
Stephano mkazi wa Ushetu alisema waligundua hali hiyo mtoto akiwa na umri wa miezi
sita lakini walishindwa kuendelea na matibabu kutokana na gharama kubwa
walizoshindwa kuzimudu.
“Tulifurahi kusikia kwamba madaktari bingwa kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete wanakuja Shinyanga, tumepata matumaini mapya na tunashukuru
kwamba sasa mjukuu wangu ana nafasi ya kufanyiwa upasuaji kwa kusaidiwa
kulipiwa matibabu hayo”.
“Tumefika hapa mtoto amepimwa lakini tundu kwenye moyo wake
bado lipo na anatakiwa kufanyiwa upasuaji, nimefurahi sana na Mungu awazidishie pale walipotoa wote
waliochangia matibabu ya moyo kwa watoto
wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchuni”, alisema Bibi Monica.
Naye mkazi wa Kishapu Lucas Marwa ambaye mtoto wake alipata huduma katika kambi hiyo alisema changamoto walizokuwa wakizipitia ni kutokupata majibu sahihi kila walipokwenda hospitalini, lakini sasa wamepata majibu mazuri na mwelekeo wa matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
“Madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametupa mwanga mpya, tunaomba wadau mbalimbali waendelee kusaidia huduma hizi kwani zinagusa maisha ya familia nyingi”, alisema Marwa.

Comments
Post a Comment