JKCI YAPOKEA MILIONI 100 KWA AJILI YA KUSAIDIA MATIBABU YA MOYO KWA WATOTO
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya hundi ya shilingi milioni 100 kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo kutoka kampuni ya ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) leo jijini Dar es Salaam.
************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) imepokea msaada wa shilingi milioni 100 kutoka kwa
kampuni ya ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa
ajili ya kusaidia watoto wadogo wenye matatizo ya moyo wanaohitaji kufanyiwa
upasuaji.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema msaada huo umeletwa katika
wakati muafaka ambapo watoto wanaohitaji upasuaji wa moyo hawana uwezo wa
kifedha.
Dkt. Kisenge
amesema kuwa msaada huo utarudisha matumaini kwa watoto na watanzania walikuwa
wanashindwa kulipa gharama za matibabu ya moyo.
“Leo tumepokea
msaada wa shilingi milioni 100 kutoka kwa wenzetu wa EACOP ambao utagharamia
upasuaji wa watoto wadogo wenye matatizo ya moyo.”
“Huu ni msaada
mkubwa unaobeba matumaini makubwa kwa familia zisizo na uwezo.” Amesema Dkt.
Kisenge.
Ameongeza kuwa
fedha hizo si tu kwamba zitasaidia watoto walio na hali mbaya bali pia
zitaongeza uwezo wa taasisi katika kutoa huduma bora na endelevu kwa watoto
wenye matatizo ya moyo.
“Kwa kuwa
upasuaji wa moyo unagharimu fedha nyingi kwa mtoto mmoja ni wazi familia nyingi
haziwezi kumudu kwa hiyo msaada huu utasaidia kurudisha maisha ya watoto
waliokuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha lakini pia tutanunua vifaa muhimu
vitakavyotumika kwenye upasuaji wa watoto.” Aliongeza Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Meneja
wa Mradi wa EACOP Tawi la Tanzania Geofrey Mponda amesema kwamba licha ya wao kujihusisha
na mradi wa bomba la mafuta wameamua kujihusisha na masuala ya afya kama sehemu
ya kuikumbuka jamii.
“Ingawa jukumu
letu ni ujenzi wa bomba la mafuta tuliona ni muhimu kugusa maisha ya watu moja
kwa moja watoto ni kundi nyeti na linapoguswa linagusa pia msingi wa taifa la
kesho.”
“Watoto
wanapozaliwa hawajui lolote kuhusu dunia hii wanapokumbwa na changamoto ya
kiafya jamii inapaswa kuwasaidia kwa kuwaponyesha watoto hawa tunawaandaa kuwa
viongozi na wataalamu wa baadaye.” Alisema Mponda.
Daktari Bingwa
wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Naizihijwa Majani amesema kuwa takribani asilimia 80 ya watoto wamezaliwa na
matatizo ya moyo.
“Karibu asilimia
80 ya watoto wanaopatiwa huduma hapa huwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo
hata hivyo wakipatiwa matibabu mapema wengi wao hupata nafuu kabisa na huishi
maisha ya kawaida.”
“Tangu tuanze
kutoa matibabu haya tumeona mabadiliko makubwa wapo waliorejea shuleni wengine
wako vyuoni na baadhi yao wanataka kuwa madaktari kama sisi, msaada huu
unabadilisha maisha ya mtoto kwa ujumla.” Alisema Dkt. Majani.
Kupitia msaada
huo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete itaweza kununua vifaa tiba kwaajili ya kuwasaidia
watoto wenye shida ya moyo.
Comments
Post a Comment