Siku mbili tu zaidi ya watu 200 watibiwa moyo kambi maalum Shinyanga
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimsikiliza mkazi wa Shinyanga aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika mkoani Shinyanga.
Afisa Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zabela Mkojera akichukua taarifa za mkazi wa Shinyanga aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (SRRH).
******************************************************************************************************************************************************************
Watu 213 wakiwemo watu wazima 190 na watoto 23 wamepata huduma za uchunguzi na
matibabu ya moyo kwa muda wa siku mbili kwenye
kambi maalumu ya matibabu inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa
Shinyanga (SRRH).
Hayo
yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo
ya kambi hiyo inayofanyika mkoani Shinyanga.
Dkt.
Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kati ya watu
waliowaona 34 walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa
na hivyo kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.
“Tumetoa
rufaa kwa watu wazima 26 na watoto nane ambao tuliwakuta na matatizo ya matundu
kwenye moyo, mioyo yao kuchoka na hivyo kushindwa kufanya kazi vizuri, moyo
kutanuka, valvu za moyo na mishipa ya damu ya moyo kuziba”, alisema Dkt.
Kisenge.
“Magonjwa
ya moyo ni magonjwa yanayoweza kuepukika endapo utafuata ushauri wa kitaalamu,
ninawaomba wananchi mzingatie kula vyakula bora ikiwemo mboga za majani na
matunda, kufanya mazoezi japo kwa kutembea dakika 150 kwa wiki, kuepuka uvutaji
wa sigara na unywaji wa pombe kupindukia”.
“Jengeni
tabia ya kupima afya zenu japo mara moja kwa mwaka, lala usingizi wa kutosha
kitaalamu inashauriwa kulala masaa saba na zuia msongo wa mawazo kwa kufanya
hivi utaepuka kupata magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema jana ni siku ya
pili tangu wameanza kambi hiyo ya matibabu aliwasihi wananchi wa mkoa wa
Shinganya na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kupima afya za mioyo yao katika
siku tatu zilizobaki na kuwaomba kutumia fursa hiyo ya thamani kwani huduma ipo karibu
na wao.
Kwa upande wa wananchi waliopata
huduma katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma hiyo na kusema kuwa imewasaidia
kufahamu afya za mioyo yao na kuwapunguzia kufuata huduma hizo jijini Dar es
Salaam.
“Ninashukuru kwa huduma niliyoipata ni
nzuri, nimefika hapa mapema nimepima vipimo vyote vya moyo na nimeonana na
mtaalamu ambaye amenipa elimu ya magonjwa ya moyo na kunianzishia dawa kwani
moyo wangu umekutwa na tatizo la kuziba kwa mshipa wa damu nimepewa rufaa ya
kwenda kutibiwa JKCI”, alisema John Jilanga mkazi wa Kahama.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea wataalamu wa moyo katika mkoa wetu wa Shinyanga, ninaomba huduma hizi ziwe endelevu pia watuletee na wataalamu wa magonjwa mengine yakiwemo ya mifupa”, alishukuru Mary Masanja mkazi wa Kishapu.
Comments
Post a Comment