JKCI yatoa elimu na huduma za afya ya moyo Zambia
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph akimkabidhi zawadi Waziri wa Fedha na Mipango wa Zambia, Mhe. Dkt. Situmbeko Musokotwane alipotembelea banda la taasisi hiyo lililopo katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph akimsikiliza Mtaalamu wa Nishati kutoka Wizara ya Fedha na Mipango ya Zambia Fabrizio Marino aliyefika katika banda la taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka kwa ajili ya kufahamu huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph akimweleza Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Dkt. Mpoki Ulisubisya huduma zinazotolewa na taasisi hiyo katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuonesha dhamira yake ya dhati ya kutoa huduma bora za matibabu ya moyo katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa kushiriki katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara yanayofanyika jijini Lusaka, Zambia.
Akizungumza na waandishi wa habari
waliofika katika banda la taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya
moyo zinazotolewa Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Alex
Joseph alisema ushiriki wa taasisi hiyo
katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za kupeleka elimu, huduma za
uchunguzi, na ushauri wa kiafya kwa wananchi wa Zambia na nchi jirani.
Dkt. Alex
alisema taasisi hiyo imekwenda Zambia siyo kwa ajili ya kutangaza huduma peke
yake bali pia kushirikiana na Hospitali ya Moyo ya Zambia katika mapambano
dhidi ya magonjwa ya moyo.
“Tumeleta
timu ya madaktari bingwa kwa watoto na watu wazima kwa ajili ya kutoa huduma ya
uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo, ushauri wa kitaalamu na kutoa elimu ya
afya ya moyo”.
“Wananchi wengi waliotembelea katika
banda letu wamepata elimu ya magonjwa ya moyo, kuna ambao tumewafanyia vipimo
vya awali vya moyo ambavyo ni shinikizo la damu na wingi wa sukari kwenye damu huku
wengine wakihamasika kujifunza kuhusu njia za kujikinga dhidi ya magonjwa ya
moyo”, alisema Dkt. Alex.
Dkt. Alex alisema JKCI pamoja na kutoa
huduma za kawaida pia inatoa huduma za matibabu katika kliniki maalum (VIP Clinic) kwa wagonjwa wa ndani ya
nchi na International Clinic kwa
wagonjwa wanaotoka nje ya Tanzania.
“Tunazo
huduma za VIP Clinic kwa wale wanaohitaji huduma za haraka vilevile
International Clinic kwa wageni kutoka nje ya nchi. Huduma hizi zimeongeza
ufanisi wa upatikanaji wa tiba ya moyo kwa watu wa mataifa mbalimbali, ikiwemo
Zambia”, alifafanua Dkt. Alex.
Baadhi ya wananchi wa Zambia waliopata
huduma katika banda hilo waliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kujali maisha ya watu bila ya kuangalia mipaka ya kitaifa iliyopo.
“Nimefurahishwa sana na huduma niliyoipata
kutoka kwa madaktari wa Tanzania, ni ya kitaalamu, ya haraka na yenye huruma, nimepewa
ushauri muhimu kuhusu namna ya kuishi maisha yenye afya ya moyo. Nashukuru sana
JKCI kwa kufika hapa Zambia”, alishukuru Joseph Banda mkazi wa Lusaka.
Naye Mary Tembo, mama wa mtoto aliyefanyiwa uchunguzi wa moyo alisema mtoto wake alikuwa analalamika maumivu ya
kifua mara kwa mara baada ya kufika katika banda hilo wamepata huduma bila
malipo kutoka kwa madaktari wa Tanzania, aliishukuru JKCI kwa moyo wa ubinadamu
walionao.
Kwa upande mwingine JKCI imetumia maonesho hayo kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa afya baina ya Tanzania na Zambia, sambamba na kuonesha uwezo wa wataalamu wake katika kutoa huduma za kibingwa bobezi ambazo zimeendelea kuokoa maisha ya maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Comments
Post a Comment