Elimu ya Lishe bora yatolewa katika maonesho ya Nanenane Dodoma
Na: Shose Romwald
***********************************************************************************************
Wakazi wa Dodoma na mikoa ya jirani wafaidika na elimu ya
lishe bora inayotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika maonesho
ya 32 ya Kitaifa ya Nanenane
Elimu hiyo imejikita kuwasaidia wananchi kubadili mtindo wa
maisha utakaowasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya
moyo yanaoongoza kwa vifo vingi duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Afisa
Lishe kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingindo alisema
huduma ya lishe ni sehemu muhimu ya matibabu kwa watu mwenye magonjwa ya moyo,
watu wenye uzito mkubwa na watu wenye tatizo la shinikizo la damu.
Lingindo alisema jamii pia inatakiwa kuacha matumizi ya sigara
na unywaji wa pombe uliokithiri kwani kwa kutumia vilevi hivyo pia wapo katika
hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Katika maonesho haya ya Nanenane hadi leo tumeweza kutoa
elimu ya lishe bora kwa wananchi 70 ambapo kati yao wapo tuliowakuta na uzito
mkubwa, shinikizo la damu na wengine wanaotumia vilevi kupindukia, kama
watafuata ushauri wetu watakuwa salama”, alisema Lingindo.
Kwa upande wake mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo
Rehema Msemwa alisema elimu aliyopata kuhusu lishe itamsaidia kupunguza uzito wake
ili aweze kuulinda moyo wake usipate madhara yanayoweza kusababishwa na uzito
mkubwa na mafuta mengi mwilini.
“Nimekuwa nikila chakula bila kuzingatia mlo kamili na muda
sahihi wa kupata chakula hivyo kunipelekea kupata uzito mkubwa, baada ya kupata
elimu hii ninaenda kuzingatia mlo kamili na kuongeza ulaji wa mbogamboga na
matunda katika chakula changu”. alisema
Rehema.
Naye Hassani Magesa mkazi wa Dodoma aliishauri JKCI kutoa
elimu ya lishe bora wananchi kupitia vipindi vya Redio na Televisheni ili
waweze kuisaidia jamii kuwa na afya bora itakayowasaidia kujikinga na magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Nimeshauriwa katika sahani yangu ya chakula nihakikishe
nakula mbogamboga nyingi, matunda, vyakula vyenye protini na wanga kiasi huku
nikiepuka kula vyakula vyenye mafuta mengi, lakini pia nimehaswa kufanya
mazoezi ya mwili angalau dakika 30 kwa siku mwili wangu uweze kukaa katika hali
ya afya nzuri”, alisema Magesa
Comments
Post a Comment