Shinyanga waitwa kupima moyo

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimsikiliza mwananchi aliyefika katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga (SRRH) kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo. Kushoto ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga (SRRH) Dkt. Luzila Boshi akifuatiwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga (RMO) Dkt. Yudas Ndungile.
*****************************************************************************************************************************
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi zawadi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga alipomtembelea ofisini kwake leo kabla ya kuanza kwa kambi maalumu ya siku tano ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga (SRRH).
Wakazi wa mkoa wa Shinyanga na mikoa ya jirani wametakiwa
kujitokeza kwa wingi kupima afya za mioyo yao pamoja na saratani ya shingo ya
kizazi huduma zinazotolewa kwenye kambi maalumu ya matibabu inayofanyika katika
Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga (SRRH).
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Mboni Mhita wakati
akifungua kambi maalumu ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo na saratani
ya shingo ya kizazi inayofanyika katika Hospitali hiyo.
Mhe. Mboni alisema mkoa wa Shinyanga ni moja ya mikoa ambayo iko
mbali na Hospitali zinazotoa huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa
mbalimbali ikiwemo moyo kuwepo kwa kambi hiyo ya matibabu kutawasaidia wananchi
kupata huduma ya uchunguzi na matibabu kwa urahisi tofauti na ambavyo
wangezifuata Dar es Salaam.
“Tunaishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa ulioufanya katika
sekta ya afya hii ikiwa ni pamoja na kujenga majengo ya kisasa, kusomesha
wataalamu na kununua vifaa tiba vya kisasa, huduma za matibabu ya ubingwa bobezi
zimesogezwa karibu zaidi na wananchi hii ndiyo maana mnaona leo wataalamu wetu
wako hapa Shinyanga kutoa huduma kwa wananchi”, alisema Mhe. Mboni.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga (RMO) Dkt.
Yudas Ndungile alisema katika kambi hiyo kutakuwa na madaktari bingwa wa moyo
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambao watatoa huduma za kibingwa
za uchunguzi wa magonjwa ya moyo, elimu ya magonjwa ya moyo na kuwajengea uwezo
wataalamu wa afya kutoka hospitali zote za wilaya za mkoa huu.
“Pia tuko na wataalamu kutoka Hospitali ya Aga Khan ya jijini
Dar es Salaam ambao wanatoa huduma za uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi,
elimu ya magonjwa ya saratani, pamoja na matibabu ya awali ya ugonjwa huu ambao
watakuwepo katika hospitali hii kwa muda wa wiki moja baada ya hapo watakwenda
wilaya za Shinyanga na Kahama”, alisema Dkt. Yudas Ndungile.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kutokana na tatizo la magonjwa ya moyo
ambayo yanaweza kuzuilika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu kuwa kubwa na
kusababisha vifo vya watu wengi, JKCI ilianzisha program ya Tiba Mkoba ya Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kwa kusogeza huduma za ubingwa
bobezi kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo.
“Katika program hii tunashirikiana na wataalamu
wa Hospitali za Kanda, Mikoa, Wilaya na Vituo vya Afya kutoa huduma za
uchunguzi na matibabu ya moyo, elimu ya lishe bora na matumizi sahihi ya dawa
za moyo kwa wananchi. Tunawajengea uwezo wataalamu wa Afya wa kutambua na
kutibu magonjwa ya moyo ili watakapowapata wagonjwa waweze kuwapa matibabu
sahihi na kwa wakati”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema tangu program hiyo
imeanza mwaka 2022 wameshatoa huduma katika mikoa 21 na maeneo ya kazi 17 na
kuwafikia watu 35,456 watu wazima wakiwa 32,345 na watoto 3,111 kati ya hao 12,685 watu wazima wakiwa 12,164 na watoto 521 walikutwa na matatizo
mbalimbali ya moyo na kuanzishiwa matibabu.
“Katika ya watu tuliowaona wagonjwa 3,199 watu wazima 2,857 na watoto 342 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI” alisema Dkt.Kisenge.
Comments
Post a Comment