JKCI kufanya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 10 ya JKCI uliofanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
Baadhi ya viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 10 ya JKCI uliofanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
**********************************************************************************************************
Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuadhimisha miaka 10
tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya kampeni maalumu ya uhamasishaji wa magonjwa
ya moyo nchini.
Maadhimisho hayo yanaanza rasmi tarehe 1 mwezi Agosti na
kuhitimishwa tarehe 20 Septemba mwaka huu yatahusisha mhadhara wa umma
kujadiliana kuhusu tiba utalii nchini pamoja na kufanya bonanza la wafanyakazi
wa Taasisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar
es saalamu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Peter Kisenge alisema Taasisi hiyo inaadhimisha miaka 10 kutokana na mafanikio
iliyoyapata katika kutoa huduma bingwa bobezi za uchunguzi na matibabu ya moyo
nchini.
Dkt. Kisenge alisema kwa kipindi cha miaka 10 JKCI imeweza kutoa
huduma za upasuaji wa moyo wa kisasa kupitia mtambo wa Cathlab (Catheterization
Laboratory) na kuweza kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve)
bila kufungua kifua.
Mafanikio mengine ambayo taasisi hiyo imeyapata ni pamoja na
kuongeza utaalamu katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo, kuanzisha program za
uhamasishaji na uchunguzi kupitia huduma ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, kushirikiana na mataifa mbalimbali duniani, kufanya tafiti na
mafunzo kwa wataalamu wa afya pamoja na kuwekeza katika vifaa tiba vya kisasa.
Aidha Dkt. Kisenge alisema JKCI katika kuendelea kuboresha
huduma za matibabu ya moyo imeweka mikakati ya baadaye ikiwemo kuwa na jengo la
watoto wenye matatizo ya moyo eneo la Mloganzila, kuimarisha huduma kwa
kuongeza huduma za matibabu ya moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato,
Lumumba Zanzibar, na Arusha Lutheran (Seriani), kuendeleza utafiti pamoja na
kupandikiza moyo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa maadhimisho ya miaka 10 ya JKCI
Dkt. Naizihijwa Majani alisema kampeni zinazofanywa na Taasisi hiyo wakati wa
kuadhimisha miaka 10 ya JKCI zitaenda sambamba na kampeni ya kuzuia magonjwa ya
moyo kwa watoto kwa kutoa elimu ya afya na uchunguzi wa moyo kwa wanafunzi
katika shule za sekondari.
Dkt. Naizihijwa alisema katika mhadhara utakaofanyika wakati
wa maadhimisho hayo JKCI imepanga kujadili umuhimu wa tiba utalii nchini na
manufaa yake kwa wananchi, nafasi ya mashirika ya umma katika tiba utalii
pamoja na mafanikio ya tiba utalii baada ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
“Mhadhara utakaofanywa na Taasisi yetu kuhusu tiba utalii
nchini utaongozwa na wataalamu bobebi kutoka sekta ya afya pamoja na sekta ya
utalii nchini”, alisema Dkt. Naizihijwa
Maadhimisho ya miaka 10 ya JKCI yenye kauli mbiu
“Tumethubutu, Tumeweza Tunasonga mbele” yanatarajiwa kuambatana na matukio
mbalimbali ya kitaaluma, utafiti, huduma za kijamii, pamoja na uzinduzi wa
mikakati mipya ya kuboresha huduma za moyo nchini.
Comments
Post a Comment