Wanafunzi 2,328 wapimwa moyo Kibaha
Daktari bingwa wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) Theophil Ludovic akiwafundisha wanafunzi wa Shule ya Msingi Mailimoja kuhusu magonjwa ya moyo kwa watoto wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanywa na Taasisi hiyo katika maadhimisho ya miaka 10 ya JKCI tangu kuanzishwa kwake.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya
Moyo Jakaya kikwete (JKCI) Stella Mongela akimpima kipimo cha kuangalia jinsi
moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) mwanafunzi wa Shule ya Msingi
Mailimoja wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanywa na Taasisi hiyo katika maadhimisho ya
miaka 10 ya JKCI tangu kuanzishwa kwake.
Na JKCI
******************************************************************************************************
Wanafunzi 2,328 kutoka Shule ya Msingi Mailimoja na Sekondari
ya Bundikani zilizopo Wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani wamefanyiwa uchunguzi wa awali
wa magonjwa ya moyo.
Upimaji huo umefanyika katika kambi maalumu ya siku mbili ya
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi hiyo tangu
kuanzishwa kwake.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo Daktari bingwa
wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella
Mongela alisema watoto sita wamepatiwa rufaa kufika JKCI kwaajili ya uchunguzi
zaidi na watoto wawili wamepewa rufaa kufika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani
(Tumbi).
Dkt. Stella alisema baada ya wanafunzi hao kufanyiwa kipimo
cha kuangalia mapigo yao ya moyo wanafunzi 34 waliokuwa na viashiria vya
magonjwa ya moyo walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiography) ambapo watoto sita walikutwa na magonjwa ya moyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi waliofanyiwa
upimaji huo wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwafikia na
kuwapa elimu kuhusu magonjwa ya moyo.
Shania Hassan wa shule ya Sekondari Bundikani alisema hapo
awali hakuwa na elimu kuhusu magonjwa ya moyo lakini kupitia kambi hiyo ameweza
kupata elimu ambayo itamsaidia kujikinga na magonjwa hayo.
“Tumesisitizwa kufanya mazoezi kwa afya, leo nimepata nafasi
ya kujua umuhimu wa kufanya mazoezi, lakini pia nimejua mazoezi ni sehemu ya
kinga dhidi ya magonjwa ya moyo”, alisema Shania.
Naye Emmanuel Mangano aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuwafuata
na kuwapa huduma hivyo kuiombea Taasisi hiyo iendelee kufanikiwa zaidi katika
kutoa huduma za matibabu ya moyo.
“Leo nimefurahi sana nimepata elimu nzuri kuhusu magonjwa ya
moyo, Taasisi hii inavyoendelea kutoa huduma za upasuaji wa moyo iendelee
kufanikiwa na kujulikana zaidi”. Alisema Emmanuel
Comments
Post a Comment