JKCI yashinda tuzo ya uboreshaji wa huduma za matibabu ya moyo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge tuzo ya mshindi wa kwanza katika uboreshaji wa utoaji huduma. Tuzo hiyo imetolewa leo katika kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kinachofanyia kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kilichopo jijini Arusha.
*********************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepata tuzo
ya mshindi wa kwanza katika uboreshaji wa utoaji huduma za afya ikiwa ni ishara
ya mafanikio yake katika kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini.
Tuzo hiyo imetolewa leo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango katika kikao kazi cha Wenyeviti
wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kinachofanyia katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kilichopo jijini Arusha.
Akizungumza wakati akikabidhi tuzo hiyo Mhe. Mpango
aliipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma inazozitoa za
matibabu ya moyo kwa wagonjwa.
Akizungumza kabla ya kutolewa kwa tuzo hiyo ya uboreshaji wa utoaji
wa huduma Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu alisema katika tuzo hizo walikuwa
wanaangalia uboreshaji wa huduma na matumizi ya teknolojia ya kidijitali,
kuridhika kwa wateja katika upatikanaji wa huduma na kuongezeka kwa wateja
ambapo JKCI ilishika nafasi ya kwanza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Peter Kisenge alishukuru kwa tuzo waliyopewa na kusema kuwa taasisi
hiyo itaendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa inaowahudumia pia itaangalia
namna itakavyozidi kutanua huduma zake.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema JKCI inashiriki katika kikao kazi cha tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji
Wakuu wa Taasisi za Umma kwa kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu
ya moyo.
“Viongozi wengi wana majukumu mengi ya kazi na kukosa muda wa
kwenda hospitali kupima afya zao, wataalamu wa JKCI tumeona tuwafuate katika
kikao hiki ili wakati wa mapumziko waje kupima afya za mioyo yao”.
Katika upimaji huu tunashirikiana na wenzetu wa Hospitali ya
AICC na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kutoa huduma
mbalimbali za matibabu na ushauri zikiwemo za moyo, ubongo, mgongo, viungo vya
mwili, mifupa na mishipa ya fahamu pamoja na kufanya vipimo vya maabara ambapo
majibu yao wanayapata ndani ya muda mfupi.
Dkt. Kisenge alisema wale wanaowakuta na shida wanawaanzishia matibabu kwa kuwapa dawa na wengine wanawapa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI au MOI kutokana na shida walizokuwa nazo.
Comments
Post a Comment