Wananchi Dodoma kupimwa Moyo Maonesho ya 32 ya Nanenane
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Johnstone Kayandabila akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 32 ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Afisa Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Loveness Mfanga akichukuwa taarifa za mkazi wa Dodoma aliyefika katika banda la
Taasisi hiyo kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa
Maonesho ya 32 ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini
Dodoma.
Na: Shose Romwald
****************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatoa huduma za
upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Dodoma wakati wa maonesho ya 32 ya
kitaifa ya Nanenane yanayofanyika jijini humo.
Upimaji huo unafanyika bila gharama kwa wananchi wote
watakaotembelea banda la Taasisi hiyo lililopo katika maonesho hayo
yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni vilivyopo jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Johnstone
Kayandabila alisema JKCI itatoa huduma ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa
kuwafanyia wananchi kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiography – ECHO), kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo
(Electrocardiography – ECG), kipimo cha kuangalia shinikizo la damu, kipimo cha
kuangalia sukari kwenye damu pamoja na ushauri wa lishe kutoka kwa Afisa lishe.
Dkt. Kayandabila aliwataka wananchi wasiwe na hofu ya kufanya
vipimo vya moyo kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kubadilisha mtindo wa
maisha, lakini pia kuweza kukabiliana na athari za magonjwa ya moyo zinazotokea
wakati wowote.
“Kinga ni bora kuliko tiba, JKCI tunaisaidia jamii kupata
uelewa kuhusu magonjwa ya shinikizo la damu na magonjwa ya moyo, kufuata
ushauri wa kitaalamu kuhusu lishe bora kwani magonjwa haya mara nyingi hutokana
na ulaji usiofaa” alisema Dkt. Kayandabila
Kwa upande wake Dickson Mkuyu mwananchi aliyetembelea banda
hilo alisema baada ya kupate elimu ya mfumo bora wa maisha ataenda kubadilisha
mfumo wake wa maisha ili aweze kujikinga na magonjwa ya moyo.
“Ni vyema jamii ikatumia fursa hii kujua afya zao na kupata
ushauri kutoka kwa madktari wabobezi wa magonjwa ya moyo, hii itatusaidia
kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yetu “alisema Mkuyu
Naye Mary Kitoi mkazi wa Dodoma aliyefanyiwa vipimo vya moyo
katika banda hilo alisema ameshauriwa kuwa anafanya uchunguzi wa afya mara kwa
mara utakaomsaidia kuchukua hatua za haraka pale atakapokutwa na changamoto
yoyote ya kiafya.
“Nimekuwa nikijitahidi sana kufanya mazoezi kuuweka mwili
wangu kuwa na nguvu lakini nimekuwa pia nikijitahidi kula mlo unaohusisha
makundi mbalimbali ya vyakula hivyo kama nitaendelea na mtindo huu wa maisha
nitajilinda na maognjwa ya moyo”, alisema Mary
Comments
Post a Comment