Kambi ya matibabu ya moyo yaacha tabasamu kwa wananchi wa Shinyanga

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi dawa mkazi wa Shinyanga aliyefika katika Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga (SRRH) kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa hivi karibuni na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa SRRH.

Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Paskal Kondi akimfanyia mwananchi kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku tano iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga (SRRH).
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce akizungumza na mwananchi wa Shinyanga kuhusu matumizi sahihi ya dawa wakati wa kambi maalumu ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kiketwe (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH).
Baadhi ya wakazi wa Shinyanga wakisubiri kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga (SRRH) wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyomalizika hivi karibuni.
**********************************************************************************************************************************************************************
Watu 502 wamepata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalum ya matibabu iliyofanyika kwa siku tano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH).
Kambi hiyo ilifanywa na
wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH).
Akizungumza na waandishi wa
habari hivi karibuni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga
(SRRH) Dkt. Luzila John alisema kati ya watu waliowaona watu wazima walikuwa 437
na watoto 65.
“Watu wote hawa walifanyiwa
vipimo vya maabara vya kuangalia matatizo mbalimbali yanayoweza kusababisha
magonjwa ya moyo. Watu 328 tuliwafanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya
kazi na watu 287 waliwafanyia kipimo cha
kuangalia mfumo wa umeme wa moyo”.
“Kati ya wagonjwa tuliowaona
kuna ambao walikutwa na matatizo makubwa ya moyo ambayo yalihitaji matibabu ya
kibingwa hivyo tumewapa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI, idadi yao ni 100 watu wazima wakiwa 63 na watoto 37”,
alisema Dkt. John.
Dkt. John alisema lengo la
kambi hiyo ilikuwa ni kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo karibu zaidi
na wananchi wa mkoa wa Shinyanga ili kuwapunguzia gharama za usafiri za kwenda
Dar es Salaam.
“Wataalamu wetu wa afya wapatao 16 wamepata mafunzo ya namna ya
kufanya uchunguzi wa moyo na kutoa huduma za awali, hii ni fursa muhimu kwa
hospitali ya mkoa na halmashauri za mkoa wa Shinyanga”, alisema Dkt. John.
Kwa upande wake daktari
bingwa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, Mlagwa
Yango alisema wagonjwa wengi waliwakuta na tatizo la Shinikizo la juu la damu, moyo
kutanuna, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri, matatizo ya valvu, mishipa ya
damu ya moyo na matundu kwa watoto.
Dkt. Yango alisema kufanyika
kwa kambi hiyo kumewasaidia wananchi
kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa haraka zaidi tofauti na
ambavyo wangezifuata Dar es Salaam kwani kuna gharama za usafiri.
“Tunapowahudumia wananchi kwa kuwafuata
mikoani mikoani tunawarahisishia kupata huduma na kupunguza idadi ya wagonjwa
wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu”, alisema Dkt. Yango.
Nao wananchi waliopata
huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi hiyo walishukuru kwa
huduma waliyoipata na kuomba huduma hiyo
ifanyike mara kwa mara.
“Huduma ni nzuri ila tunaomba ziwe endelevu, mara nyingi ni
gharama kubwa kwenda Dar es Salaam kupata huduma hizi hivyo ujio wa madaktari
bingwa unatupunguzia mzigo mkubwa wa kufuata matibabu Dar es Salaam”, alisema Damas Kimaro mkazi wa Manispaa ya
Shinyanga.
“Huduma tumepokea vizuri madaktari na wauguzi
wametuhudumia bila rushwa wala usumbufu nimefurahi na ninashukuru kwa kutuletea
huduma hizi, zimekuwa msaada mkubwa kwani wengi hatuna uwezo wa kusafiri hadi
Dar es Salaam”, alishukuru Happiness Bwire mkazi wa Majengo Mapya.
Kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo mkoani Shinyanga ni sehemu ya programu ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services yenye lengo la kuwasogezea karibu wananchi huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.



Comments
Post a Comment