JKCI yasherehekea miaka 10 kwa mdahalo wa Utalii wa Matibabu
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph akimpima Shinikizo la damu mkazi wa Zambia aliyefika katika banda la taasisi hiyo kwaajili ya kupata huduma ya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yaliyomalizika hivi karibuni jijini Lusaka. JKCI ilishiriki katika maonesho hayo kwa kwenda kutangaza huduma za matibabu ya ubingwa bobezi ya moyo inazozitoa.
********************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeandaa mdahalo wa Utalii wa Matibabu wenye lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu mchango wa taasisi hiyo katika kuboresha huduma za afya ya moyo na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka kumi tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti
wa Kamati ya maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Naiz Majani alisema mdahalo huo utafanyika
katika ukumbi wa maktaba mpya uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) tarehe
15 mwezi huu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa sita mchana.
Dkt. Naiz ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa JKCI
alisema Serikali imeboresha miundombinu ya afya hii ikiwa ni pamoja na
upatikianaji wa huduma bora za afya za
ubingwa bobezi na hivyo kuwafanya watu wengi kutoka nje ya nchi kuja kutibiwa
nchini na kukuza uchumi wa taifa.
“Katika mdahalo huu tutajadili utalii wa matibabu na manufaa yake kwa mtanzania
mmoja mmoja, utalii wa matibabu Afrika: Tulikotoka, tulipo na tunakoelekea, nafasi
ya Mashirika ya Umma katika kukuza utalii wa matibabu Tanzania na tulipofikia
Tanzania katika utalii wa matibabu”.
“Utalii wa matibabu ni fursa ya kipekee kwa watanzania wote
kukuwa kiuchumi kuanzia wamiliki wa magari ya usafirishaji, wajasiriamali wa
chakula hadi watoa huduma za malazi watakapofikia wageni kutoka nje ya nchi
ambao watakuja kutibiwa hapa nchini”, alisema Dkt. Naiz.
Dkt. Naiz aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mtahalo huo ili wajifunze namna ambavyo tiba utalii inavyoweza kuboresha maisha yao na kuinua uchumi wa taifa.


Comments
Post a Comment