Kuelekea miaka 10 ya JKCI yaweka kambi Bagamoyo kuwapima moyo wanafunzi
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theophil Ludovic akiwafundisha wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Hassanal Damji dalili za magonjwa ya moyo wakati wataalamu kutoka JKCI walipotembelea shule hiyo jana kabla ya kuanza kwa kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanyika Wilayani Bagamoyo.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prisca
Kiyuka akimfanyia uchunguzi mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Hassanal Damji
kabla ya kumfanyia vipimo vya awali vya magonjwa ya moyo wakati wa kambi
maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa wanafunzi wa shule
za msingi na sekondari ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba
mkoba inayofanyika Wilayani Bagamoyo.
Picha na JKCI
******************************************************************************************************
Katika kuadhimisha miaka 10 ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) imefanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa wanafunzi wa shule za msingi
na sekondari zilizopo Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani.
Uchunguzi huo wa magonjwa ya moyo unafanyika kwa siku mbili
kupitia kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Tiba Mkoba kuwasaidia
watoto kugundua kama wana magonjwa ya moyo na kuwaanzishia matibabu.
Akizungumza wakati wa kambi hiyo iliyoanza jana Wilayani
Bagamoyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Evelyne Fulumbe alisema JKCI inaadhimisha miaka kumi
tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya shughuli mbalimbali katika jamii ikiwemo
kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika jamii.
“Tumefika katika Wilaya ya Bagamoyo kuwapima moyo watoto
waliopo katika shule za msingi na sekondari, kikubwa tunawachunguza kama
wamepata magonjwa ya valvu za moyo yanayotokana na ugonjwa wa mafindofindo unaoweza
kupeleka athari katika milango ya moyo”, alisema Dkt. Evelyne
Dkt. Evelyne alisema katika kambi hiyo wanawachunguza
wanafunzi kama wana dalili za magonjwa ya moyo na ikitokea wapo wenye magonjwa
hayo wanawapa rufaa kufika JKCI kwaajili ya matibabu zaidi.
“Athari za magonjwa ya valvu za moyo yakichelewa kutibiwa
yanaweza kupelekea mtoto kufanyiwa upasuaji wa moyo na wakati mwingine kutumia
dawa kwa muda mrefu lakini yakiwahi kutibiwa mtoto anapata dawa za kumzuia
asipate maambukizi zaidi na anakuwa sawa”, alisema Dkt. Evelyne
Dkt. Evelyne aliwataka wazazi ambao watoto wao wamekutwa na
matatizo ya moyo kufanyia kazi maelekezo ambayo wataalamu wa JKCI wameshauri
ili watoto hao waweze kupata matibabu haraka na kuendelea na masomo yao.
Kwa upande wake Mwalimu Msaidizi wa Afya kutoka Shule ya
Sekondari ya Hassanal Damji Anitha Mlindwa alisema katika shule yake wameshakutana
na changamoto mbalimbali za watoto kuwa na magonjwa tofauti tofauti yakiwemo
magonjwa ya moyo hivyo huduma ya kuwapima watoto moyo itawasaidia kuwatambua
haraka na kuwalinda wasipate changamoto nyingine.
Mwalimu Anitha alisema shule kutokuwa na wataalamu afya ni
changamoto kwani ikitokea mtoto kapata matatizo ya afya shuleni inabidi
imruhusu aende nyumbani ili aweze kupelekwa hospitali kwaajili ya matibabu
ambapo baadhi ya wanafunzi wananunua dawa na kutumia bila ya kwenda hospitali
kufanyiwa uchunguzi.
“Tulishawahi kupata mtoto mmoja ambaye alikuwa akiziia mara
kwa na alipochunguzwa ilibainika ana tatizo la moyo hivyo kupatiwa ruhusa pindi
anapohitaji kwenda hospitali lakini tunashukuru kwani sasa amemaliza kidato cha
nne na anaendelea vizuri”, alisema Mwalimu Anitha.
Mwalimu Anitha alisema ujio wa wataalamu kutoka JKCI unaleta
matumaini kwa wanafunzo wake kwani utawasaidia kutambua kama wana shida za moyo
na kwa shule utawarahisishia walimu kutoa majukumu ya kazi kulingana na afya za
wanafunzi.
Naye Mwanafunzi wa Kidato cha Nne shule ya Sekondari ya ya
Hassanal Damji Baswary Mohamed alisema uchunguzi wa magonjwa ya moyo uliofanywa
kwa wanafunzi ni mzuri kwasababu wameweza kujua hali zao za afya hasa upande wa
moyo.
“Nawashukuru sana madaktari hawa kwa kuja kutupima moyo
imetupa hamasa yakupenda kupima afya zetu mara kwa mara”, alisema Baswary
Baswary aliomba wataalamu wengine wa afya wanaotibu magonjwa
mbalimbali kiwemo saratani, figo na magonjwa mengine yasiyoambukiza kutembelea
Wilaya ya Bagamoyo na kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa hayo kwa wanafunzi
ili waweze kujenga taifa lenye afya bora.
Comments
Post a Comment