Tanzania na Zambia Mfano wa Kuigwa Katika Ushirikiano Barani Afrika

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Amanda Anyoti akimweleza Waziri wa Utalii wa Zambia Mhe. Rodney Sikumba huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka.

 Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule akimkabidhi zawadi Waziri wa Kilimo wa Zambia Mhe. Reuben Mtolo alipotembelea banda la Tanzania lililopo katika  maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka. Tanzania inashiriki katika maonesho hayo kwa kuonesha huduma za afya na usafirishaji zinazopatikana nchini.

Waziri wa Kilimo wa Zambia Mhe. Reuben Mtolo akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kumaliza kutembelea banda la Tanzania lililopo katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule.

 Waziri wa Utalii wa Zambia Mhe. Rodney Sikumba akipokea zawadi kutoka kwa Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Amanda Anyoti alipotembelea banda la Tanzania kwaajili ya kuona huduma zinazotolewa wakati wa maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka.

 Waziri wa Utalii wa Zambia Mhe. Rodney Sikumba akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea banda la Tanzania lililopo katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka. Tanzania inashiriki katika maonesho hayo kwa kuonesha huduma za afya na usafirishaji zinazopatikana nchini.


Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph akiwaeleza wakazi wa Zambia huduma zinazotolewa na taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka.

****************************************************************************************************************************************************************************************

Ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Zambia umezifanya nchi hizo kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika kuimarisha mahusiano ya kijirani, kiuchumi na kijamii.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Utalii wa Zambia, Mhe. Rodney Sikumba alipotembelea banda la Tanzania katika Maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayoendelea jijini Lusaka, kwa lengo la kujionea huduma za afya na usafirishaji zinazotolewa na taasisi mbalimbali kutoka Tanzania.

Mhe. Sikumba alisema Tanzania na Zambia zimeendelea kushirikiana kwa karibu katika sekta mbalimbali zikiwemo uchukuzi, usafirishaji, utalii, nishati, biashara, afya, elimu, ulinzi na usalama, hali ambayo imekuwa chachu ya kuimarisha ustawi wa wananchi wa mataifa hayo pamoja na majirani zao.

“Uwepo wa reli ya TAZARA na bomba la mafuta la TAZAMA ni vielelezo vya wazi vya ushirikiano wetu wa kihistoria. Tunashirikiana pia katika sekta ya afya ambapo wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) huja Zambia kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto katika Hospitali yetu ya Moyo”, alisema Mhe. Sikumba.

Aliongeza kuwa mahusiano ya kihistoria yaliyowekwa na waasisi wa mataifa haya Hayati  Mwalimu Julius  Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Kenneth David Kaunda wa Zambia, ni hazina kubwa inayopaswa kuenziwa na kuendelezwa kwa vizazi vijavyo.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo wa Zambia, Mhe. Reuben Mtolo, ambaye naye alitembelea banda hilo aliipongeza Tanzania kwa kushiriki katika maonesho hayo. Alisema ushiriki wa Tanzania umeongeza uelewa wa Wazambia kuhusu huduma za afya na usafirishaji zinazopatikana nchini humo.

“Kushiriki kwenu katika maonesho haya ni ishara tosha ya kuendeleza ushirikiano ulioasisiwa na viongozi wetu wa zamani, Kaunda na Nyerere. Tunathamini sana uwepo wenu”, alisema Mhe. Mtolo.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule aliwashukuru viongozi hao kwa kutembelea banda la Tanzania na kujionea huduma zinazotolewa.

“Mwaka huu tumejipanga vizuri kushiriki kikamilifu katika maonesho haya, na mwakani tutaongeza idadi ya taasisi zitakazoshiriki ili kuendelea kutangaza huduma zetu kwa undani zaidi,” alisema Mhe. Balozi Mkingule wakati akizungumza na viongozi hao.

Taasisi za serikali kutoka Tanzania zinazoshiriki  katika maonesho hayo ni pamoja na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),na Shirika la Ndege la Air Tanzania.

Lengo la ushiriki wao ni kutangaza huduma za ubingwa bobezi wa afya pamoja na huduma za usafirishaji zinazopatikana nchini Tanzania kwa lengo la kuvutia wananchi na taasisi kutoka Zambia kushirikiana na Tanzania katika nyanja hizo.



Comments

Popular posts from this blog

Wateja wa CRDB kutibiwa JKCI kwa punguzo la asilimia 50%

Wanawake wa JKCI SACCOS wanaongoza kwa kumiliki hisa

JKCI kutanua huduma za matibabu ya moyo nchini