Dkt.Kisenge aongoza wataalamu wa JKCI kutibu moyo Arusha

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpima shinikizo la juu la damu mwananchi aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa katika kambi maalumu ya matibabu inayofanyika mkoani Arusha.

*******************************************************************************************************************************************************************************************

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amewataka wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kupima afya za mioyo yao katika kambi maalumu ya matibabu  inayofanyika Arusha Lutheran Medical Centre (Selian ya mjini).

Kambi hiyo ya siku nne za tarehe 15-18 mwezi huu inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha Lutheran Medical Centre (Selian ya mjini) ina lengo la kusogeza kwa karibu zaidi huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi.

Akizungumza kuhusu kambi hiyo Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu alisema yeye na wataalamu wenzake wabobezi wa magonjwa ya moyo pamoja na mashine za kisasa za kupima moyo ili kuona kama una shida au la wako Arusha Lutheran Medical Centre kwaajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

“Tunaanza kutoa huduma saa 2 asubuhi hadi saa 10 jioni kwa siku ya kwanza ya leo tumeona watu 100, baadhi yao tumewakuta na shida ya shinikizo la juu la damu na wengine wameshapata madhara ya ugonjwa huu hii ikiwa ni pamoja na moyo kutanuka”.

“Wagonjwa tuliowaona wengi wao ni watu wazima zaidi ya miaka 50  kwa wale tunaowakuta na matatizo makubwa yanayohitaji utaalamu zaidi tunawapa rufaa ya kuja katika taasisi yetu kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi kupitia mashine zetu za kisasa tulizonazo na kupata matibabu zaidi”, alisema Dkt. Kisenge.

Mkurugenzi huyo Mtendaji aliwahisi wananchi kufuata mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi, kutokunywa pombe kupitiza, kuacha kutumia bidhaa aina ya tumbaku na kula vyakula bora zikiwemo mboga za majani na matunda ili wajiepushe na magonjwa ya moyo.

Kwa upande wa wananchi waliopata huduma za uchunguzi na matibabu katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma hiyo na kusema kuwa imewapunguzia gharama ya kuifuata jijini Dar es Salaam.

Dorca Mbaga mkazi wa Arusha ambaye alifanyiwa upasuaji JKCI wa kubalidilishiwa valvu moja na kurekebishiwa valvu moja (Valve replacement na Valve repair) mwaka 2014 alisema alikwenda hospitalini hapo kwaajili ya kupima kipimo cha kuangalia wepesi au uzito wa damu (International Normalized Ratio - INR) ili aende nacho hospitali ya KCMC kwaajili ya kuchukuwa dawa za kulainisha damu anazotumia kila siku.

 “Baada ya kufika hapa na kuchukuwa majibu ya vipimo vya damu nikasikia wataalamu wa JKCI wako hapa, nilifurahi sana kwakuwa safari yangu ya KCMC haitakuwepo tena kwani nitatibiwa hapa na wataalamu hawa ambao wananitibu JKCI”, alisema Dorca.

Joseph Chacha mkazi wa Mara alisema yeye alisikia wataalamu wa JKCI watakuwepo Arusha na kuamua kufunga safari ya kuwafuata kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupata huduma ya matibabu ya moyo.

“Kutoka Arusha hadi Mara ni karibu zaidi ukilinganisha na umbali uliopo wa kutoka Mara hadi Dar es Salaam nimeona nitumie nafasi hii kuja kutibiwa hapa, ninaomba huduma kama hizi zizunguke  mikoa yote Tanzania kwa kufanya hivi wananchi wengi zaidi hasa wagonjwa wa moyo watafaidika nazo”, alisema Chacha.


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)