Mashine za kisasa kutumika kuchunguza moyo Geita
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete na mwenzake kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda
Chato (CZRH) Liberius Libent wakimfanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi mwananchi aliyetembelea banda la JKCI na CZRRH kliniki ya moyo
wakati wa maonesho ya 7 ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja
vya bombambili Mkoani Geita.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Michael Lazaro akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyetembelea banda la JKCI
– Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Kliniki ya moyo leo wakati wa maonesho ya 7
ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya bombambili Mkoani
Geita.
Afisa Utafiti na Mafunzo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Makrina Komba akimpima urefu na uzito mwananchi aliyetembelea banda la
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Kliniki ya
Moyo wakati wa maonesho ya 7 ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja
vya bombambili Mkoani Geita.
Na: JKCI
********************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Rufaa Kanda ya
Chato kliniki ya moyo kutumia mashine za kisasa zenye uwezo wa kuchunguza
magonjwa yote ya moyo kwa asilimia 95 wakati wa maonesho ya 7 ya teknolojia ya
madini yanayofanyika katika viwanja vya Bombambili vilivyopo mjini Geita.
Uchunguzi huo unafanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda
Chato (CZRRH) ikiwa ni muendelezo ya kuboresha kliniki ya matibabu ya moyo
katika mkoa wa Geita.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geita Daktari
bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete
alisema JKCI inafanya huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika mikoa ya
pembezoni mwa Tanzania kuwasogezea huduma wananchi wa Tanzania na nchi za
jirani kwani Tanzania ni nchi iliyopewa jukumu la kutoa huduma za kibingwa za
matibabu ya moyo Afrika Mashariki na kati.
Dkt. Salehe alisema katika maonesho hayo asilimia kubwa ya
watu waliofika katika banda la JKCI wana maradhi ya moyo katika hatua mbalimbali
yakiongoza matatizo la shinikizo la juu la damu.
“Watu tunaowaona katika banda letu wapo ambao wana matatizo
ya shinikizo la juu la damu bila ya wao kujua lakini wengine wana matatizo hayo
na wameacha kutumia dawa kwa sababu mbalimbali”,
“Wito wetu kwa jamii pale wanapogundulika kuwa na magonjwa ya
moyo wafuate ushauri wa wataalamu wa afya wa kutumia dawa na kuudhuruia kliniki
kwani magonjwa ya moyo ni chanzo cha vifo vya umri mdogo ambavyo utokea kwa
watu wenye umri kati ya miaka 30 hadi 70”, alisema Dkt. Salehe
Kwa upande wake Daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda
Chato (CZRRH) Liberius Libent alisema ushirikiano kati ya JKCI na CZRRH ulianza
mwaka 2022 lengo likiwa kuikuza, kuilea na kuiongezea uwezo Hospitali ya Rufaa
ya Kanda Chato katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu bobezi ya moyo.
Dkt. Liberius alisema ushirikiano huo umeiwezesha hosptilia
ya Kufaa ya Kanda Chato kutoa huduma za upasuaji wa mishipa ya damu ambapo hadi
sasa wameweza kuwafanyia upasuaji huo wagonjwa wanne.
“Kupitia kliniki yetu hii ya moyo kila mwezi wataalamu wa
JKCI wanafika CZRRH kuhudumia wagonjwa wa moyo na kupunguza rufaa za wagonjwa
kufuata huduma mbali na mahali wanapoishi”, alisema Dkt. Liberius
Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika banda la JKCI Robert
Nangu ameipongeza JKCI na CZRRH kwa kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya
moyo kwa wananchi kwani huduma hizo upatikana kwa nadra.
“Watanzania wengi tunasumbuliwa na maradhi ya moyo ambayo
mara nyingi upelekea kupoteza maisha bila kujua, tukipata nafasi kama hii ya
kufikiwa na huduma hizi tusijiulize mara mbili tujitokeze kupima afya zetu”,
alisema Robert
Robert alisema Serikali imeona tatizo la maradhi ya moyo
linaongezeka kwa kasi hivyo kuwekeza katika matibabu ya magonjwa hayo na
kuwafikia wananchi mara kwa mara.
Comments
Post a Comment