Wananchi washukuru kuwepo kwa kliniki ya moyo maonesho ya madini Geita

Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba akimsikiliza daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete alipotembelea banda la JKCI – Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kliniki ya moyo wakati wa maonesho ya 7 ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya bombambili Mkoani Geita.

Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli Mpiga akiwafundisha wanafunzi wa shule ya sekondari Shantamine jinsi moyo unavyofanya kazi walipotembelea banda la JKCI – Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Kliniki ya moyo wakati wa maonesho ya 7 ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya bombambili Mkoani Geita.

Afisa Utafiti na Mafunzo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Makrina Komba akimuuliza maswali ya ufahamu mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Kliniki ya Moyo wakati wa maonesho ya 7 ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya bombambili Mkoani Geita.

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Geita wakiwa katika foleni ya kupata huduma za matibabu ya moyo katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Kliniki ya moyo wakati wa maonesho ya 7 ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya bombambili Mkoani Geita.

Na: JKCI

****************************************************************************************************************

Wananchi wa Mkoa wa Geita wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Kliniki ya moyo kwa kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 7 ya teknolojia ya madini.

Pongezi hizo zimetolewa na wananchi mbalimbali waliofika katika banda la JKCI na kupata huduma za vipimo vya sukari kwenye damu, shinikizo la damu, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo.

Grace Lameck mkazi wa Mwatulole Geita alisema amefika katika maonesho hayo kwaajili ya kupima moyo wake baada ya kupata taarifa ya uwepo wa huduma hiyo ya uchunguzi wa moyo katika maonesho hayo.

Joyce alisema kutokana na hali yake ya shinikizo la damu kuwa juu alikuwa akitamani kupima moyo kwa muda mrefu lakini kutokana na changamto za maisha hakuweza kupima moyo wake.

“Nashukuru baada ya kufanyiwa vipimo vya moyo nimekutwa moyo wangu uko sawa sina tatizo lolote hivyo naahidi kufuata elimu ya mfumo bora wa maisha niliyoipata hapa”, alisema Joyce

Kayawa Mombeki mkazi wa Sengerema alisema amefurahishwa na utaratibu unaofanyika katika banda la JKCI kwani kila mtu anayefika kwaajili ya kupima moyo anapewa muda wake hivyo kupunguza msongamano katika banda.

Kayawa alisema kuwepo kwa utaratibu huo kumewafanya wananchi kupata muda mzuri wa kuongea na wataalamu wa afya kwa karibu na pale changamoto ya afya inapobainika kupewa tiba sahihi.

Naye Marietha Maduhu ameushukuru uongozi wa mkoa wa Geita kwa kuwezesha maonesho hayo kufanyika kwani kupitia maonesho hayo wameweza kupata nafasi ya kutibawa na wataalamu mabingwa wa moyo.

“Tunaushukuru sana uongozi wa Mkoa kuwezesha maonesho haya na kufanikisha wataalamu wa JKCI kuja kutupima moyo kwani sisi wananchi tunaiamini sana Taasisi hiii kutokana na huduma zake za kibingwa zinazokidhi viwango vya Afrika Mashariki na kati”, alisema Marietha

Marietha alisema huduma za afya kutoka katika taasisi tofauti za afya zipewe kipaumbele katika maonesho hayo ili wananchi wapate nafasi ya kufanya uchunguzi wa magonjwa yote kupitia maonesho ya teknolojia ya madini.

 *******************************************************************************************************************************

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024