Wagonjwa wa moyo kutoka Malawi kutibiwa JKCI
Daktari bingwa wa wagonjwa wa dharura na mahututi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Vivian Mlawi akimweleza Waziri wa Afya wa Serikali ya Jamhuri ya Malawi Mhe. Khumbize Kandodo Chiponda huduma wanazozitoa kwa watoto waliolazwa katika wodi ya uangalizi maalumu (ICU) alipotembelea taasisi hiyo jana kwaajili ya kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Waziri wa Afya wa Serikali
ya Jamhuri ya Malawi Mhe. Khumbize Kandodo Chiponda akisikiliza daktari bingwa
wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau alipotembelea taasisi hiyo jana kwaajili
ya kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akizungumza na Waziri wa Afya wa Serikali ya Jamhuri ya Malawi Mhe. Khumbize Kandodo Chiponda alipotembelea taasisi hiyo jana kwaajili ya kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Jamhuri ya Malawi Mhe. Khumbize Kandodo Chiponda akizungumza na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Khuzeima Kanbhai alipotembelea taasisi hiyo jana kwaajili ya kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Jamhuri ya Malawi Mhe.Khumbize Kandodo Chiponda akiwa katika picha ya pamoja na balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes Kayola na Mkurugenzi wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya na viongozi wa JKCI mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea Taasisi hiyo na kuona namna ambavyo watawatuma wagonjwa kutoka nchi hiyo kwenda kutibiwa JKCI.
Picha na Khamisi Mussa
***************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Na Khamisi Mussa - Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Malawi imeahidi kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili wagonjwa wa moyo waliopo nchini humo hasa watoto kwenda kutibiwa katika taasisi hiyo.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya wa
nchi hiyo Mhe. Khumbize Kandodo Chiponda alipotembelea taasisi hiyo kwaajili ya
kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Mhe. waziri Chiponda ambaye pia kitaaluma ni mfamasia alisema
ameridhika na huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa kwani ameona vifaa vya
kisasa vya matibabu ya moyo, amekutana na wataalamu wabobezi ambao wanatibu
moyo na kuipongeza JKCI kwa kuokoa maisha ya wagonjwa wenye matatizo ya moyo.
“Nimefurahi sana
kufika hapa nimeona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali yenu pamoja na huduma
inayotolewa ni jambo la kufurahi na kushangaa kuona huduma hii inapatikana
Afrika tena katika nchi jirani ya Tanzania, tukirudi nyumbani tutaona namna ya
kuwa na makubaliano na taasisi hii ili wagonjwa wetu waje kutibiwa hapa hasa
watoto”.
“Ninawashukuru wataalamu wa taasisi hii kwani mmekuwa
mkiwahudumia wagonjwa kutoka nchini Malawi ninawaomba mzidi kuwahudumia kwani
tunahitaji msaada wenu tunafurahi kuona baada ya kupata matibabu wagonjwa
wanarudi nyumbani wakiwa na furaha. Pia ninawaomba mje nchini kwetu japo kwa
wiki mbili kufanya kambi za matibabu ili kuwasaidia watu wenye matatizo ya moyo”,
alisema waziri Chiponda.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo
Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo Dkt. Angela Muhozya alimshukuru
waziri huyo kwa kutembelea JKCI na kusema kuwa watahakikisha wanatoa huduma ya
matibabu ya moyo kwa wananchi wa Malawi wenye matatizo hayo.
Dkt. Angela alisema mwaka jana wataalamu wa taasisi hiyo
walikwenda nchini Malawi katika hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo katika nchi hiyo kufanya kambi maalumu ya
upimaji na matibabu ya moyo ambapo waliona watu 724 kati ya hao waliokuwa na
matatizo ya moyo walikuwa 537.
“Taasisi yetu imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi
mbalimbali za Afrika hasa zile tunazopakana nazo mipaka ikiwemo ya Malawi hadi
sasa tumeona wagonjwa 33 kutoka nchini hiyo ambapo watu wazima walikuwa 22 na watoto
11”.
“Licha ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo taasisi yetu pia
inatoa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wa afya, ninawaomba muwatume madaktari
na wauguzi na wataalamu wa vifaa tiba vya moyo waje kujifunza jinsi ya kuwahudumia
wagonjwa wa moyo pamoja na kutumia vifaa hivyo”, alisema Dkt.Angela.
Kwa upande wake balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes
Kayola alisema wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kutangaza diplomasia ya
uchumi inayojumuisha mipango ya kuinufaisha nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa.
“Wenzetu kutoka nchini Malawi wamekuja Tanzania kuhudhuria
mkutano wa MERCK Foundation nasi tukaona tutumie nafasi hii kuwaleta JKCI ili
waone huduma za matibabu ya moyo tunazozitoa, wamefika hapa wameziona na
kuzitambua hii itasaidia kuwashawishi wamalawi kuja kutibiwa moyo nchini kwetu”,
alisema Mhe. Balozi Agnes.
Mhe. Balozi Agnes alisema Tanzania imepiga hatua katika sekta ya afya kwani wananchi wanapata kwa karibu huduma za kibingwa za matibabu wao kama ubalozi wataendelea kuwashawishi wamalawi kuja kutumia huduma za matibabu ya zilizopo nchini.
Comments
Post a Comment