Wahariri wahimizwa kuelimisha jamii kupambana na magonjwa ya moyo
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari waliofika katika Taasisi hiyo Kliniki ya Kawe kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo jana jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus
Balile akitoa neno la shukrani baada ya wahariri wa vyombo vya habari nchini
kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
Kliniki ya Kawe jana jijini Dar es Salaam.
Afisa Huduma kwa Wateja wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kliniki ya Kawe Zainabu Waziri akimpatia maelekezo Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Bakari Machumu alipofika katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo uliokuwa ukifanywa kwa wahariri wa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Marsia Tillya akimfanyia kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography ECHO) mhariri wa habari
wakati wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari walivyofanyiwa uchunguzi wa
magonjwa ya moyo jana katika kliniki ya JKCI iliyopo Kawe jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda akimfanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mtoto aliyefika katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
*************************************************************************************************************
Wahariri wa vyombo vya habari nchini wametakiwa kutumia
vyombo hivyo kuihamasisha jamii kufanya uchunguzi wa afya upande wa magonjwa
yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo.
Rai hiyo imetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu alipokuwa
akiongea na wahariri hao waliofika kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika
Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe jijini Dar es Salaam.
Dkt. Shemu alisema magonjwa ya moyo yanaua kwa kasi hivyo
jamii ikiweza kupata elimu ya kutosha ya namna ya kutambua na kujikinga na
magonjwa hayo itaweza kuyadhibiti kwa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara
kufahamu mapema na kuzuia gharama kubwa za matibabu ambazo mtu angetumia kwa
kuchulewa kufanya uchunguzi.
“Magonjwa ya moyo huja kwakushtukiza, zaidi ya asilimia 60 ya
watu wanaopata mstuko wa moyo hupoteza maisha kutokana na kuchelewa kupata
huduma za matibabu kwa wakati”, alisema Dkt. Shemu
Aidha Dkt. Shemu ameitaka jamii pale inapokutana na
changamoto za maumivu makali upande wa kushoto wa kifua kufika hospitali mapema
kwaajili ya uchunguzi kwani maumivu hayo wakati mwingine hutokana na tatizo la
mstuko wa moyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania
(TEF) Deodatus Balile ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kuwa na
maono ya kuwafikia watu wa aina mbalimbali kuwafanyia uchunguzi wa afya kwani
bila hamasa hizo wapo watu ambao hasingepima.
Balile alisema kupitia upimaji huo wahariri zaidi ya 50 wamekutana
kwaajili ya kuangalia afya zao ambapo wapo ambao hawakuwahi katika maisha yao
kupima kipimo cha moyo hivyo kwao kuwa fursa.
“Kwakweli sisi kama wahariri tumefurahi sana kuona taasisi
hii inatujali hivyo kuweka historia kubwa katika maisha yetu kwa kufanya vipimo
hivi na kupata elimu ya kuwa tunachunguza afya zetu” alisema Balile
Aidha Balile amevitaka vyombo vya habari kuendelea kutumia
vizuri kalamu zao kufikisha elimu sahihi kuhusu afya kutoka kwa wataalamu wa
magonjwa mbalimbali hasa magonjwa yasiyoambukiza.
Naye mhariri wa gazeti la Mwananchi Lilian Timbuka alisema
gazeti hiyo limekuwa likiandika habari tofauti tofauti ikiwemo habari za kina
za afya kutoka kwa wataalamu wa afya.
“Afya tumeipa kipaumbele katika gazeti letu kwani tuna jarida
letu la afya linalotoka kila siku ya ijumaa ambalo tumekuwa tukilitumia
kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya afya”, alisema Lilian
Lilian alisema kufanya uchunguzi wa afya sio lazima hadi pale
unapoumwa bali uchunguzi huo unapaswa kufanyika mara kwa mara kufahamu vizuri
maendeleo ya mwili na kubaini changamoto mapema.
“Jamii yetu imekuwa ikionyesha mwitikio mdogo pale
zinapotokea nafasi za kufanya uchunguzi wa afya kwa uoga wa kukutwa na maradhi
dhana ambayo inapelekea kushindwa kutatua changamoto za kiafya kutokana na
kuchelewa kuzitambua”, alisema Lilian
Comments
Post a Comment