JKCI yapongezwa kuwafanyia vipimo vya moyo wachimbaji wa madini
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli Mpiga akimpima kipimo chakuangalia mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG) mwananchi aliyefika katika banda la JKCI – Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kliniki ya moyo wakati wa maonesho ya 7 ya teknolojia ya madini yaliyomalizika leo mkoani Geita.
Daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRRH) Liberius
Libent akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiography – ECHO) mwananchi aliyefika katika banda la JKCI – Hospitali
ya Rufaa ya Kanda Chato kliniki ya moyo wakati wa maonesho ya 7 ya teknolojia
ya madini yaliyomalizika leo mkoani Geita.
Na: JKCI
*********************************************************************************************************************
Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma za
upimaji wa magonjwa ya moyo pamoja na elimu ya kujikinga na magonjwa hayo kwa
wachimbaji wa madini wakati wa maonesho ya 7 ya teknolojia ya madini.
Pongezi hizo amezitoa leo wakati akifunga maonesho hayo
yaliyokuwa yakifanyika katika viwanja vya Bombambili na kumalizika leo mkoani
Geita.
Mhe. Dkt. Samia alisema kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa
ya moyo kwa wachimbaji wa madini kunawasaidia kujikinga na magonjwa hayo na
kuweza kujenga taifa lenye nguvu na afya bora.
Akitoa taarifa ya upimaji uliofanyika katika banda la JKCI –
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kliniki ya moyo Daktari bingwa wa magonjwa ya
moyo wa JKCI Dkt. Salehe Mwinchete alisema watu 856 wamefanyiwa uchunguzi na
matibabu ya magonjwa ya moyo.
Dkt. Salehe alisema upimaji huo umefanyika pia kwa watoto 41
waliokuwa na dalili mbalimbali zilizohusishwa na dalili za magonjwa ya moyo
ikiwemo kushindwa kupumua vizuri, kuchoka, kuwa na maumivu ya kifua pamoja na
tatizo la mapigo ya moyo kwenda kasi.
“Katika upimaji huu wanaume 399 sawa na asilimia 47 na wanawake
457 sawa na asilimia 53, wote hawa tuliwapatia huduma pamoja na elimu ya namna
ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo”, alisema Dkt. Salehe
Dkt. Salehe alisema watu 631 walifanyiwa kipimo cha kuangalia
jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) na watu 612 walifanyiwa
kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG).
“Tumetoa rufaa kwa watu wazima 235 ambapo kati yao watu 182 wanatakiwa
kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato na watu 42 Kwenda JKCI kwaajili ya
kufanyiwa vipimo vingine vya moyo pamoja na matibabu. Pia tumetoa rufaa 11 za
watoto wanaotakiwa kufika JKCI kwaajili ya matibabu na wengine kwaajili ya
kufanyiwa upasuaji wa moyo”, alisema Dkt. Salehe
Dkt. Salehe alisema watu waliofanyiwa vipimo katika banda la
JKCI wengi wao wamekutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, huku wengine
wakiwa na matatizo ya sukari kwenye damu, moyo kutanuka, matatizo ya mfumo wa
umeme wa moyo, tatizo la shinikizo la juu la damu kwenye mapafu, matatizo ya
moyo kushindwa kufanya kazi, na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo kwa watoto.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliofanyiwa
uchunguzi katika banda la JKCI Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kliniki ya
moyo wameishukuru Serikali kwa kuwekeza katika utoaji wa huduma za matibabu ya
moyo nchini.
Mathayo Martine alisema ikiwezekana huduma za uchunguzi wa
magonjwa ya moyo zinazofanywa na JKCI zisiishie katika maonesho hayo bali
ziendelee kutolewa mara kwa mara kwani uhitaji wa huduma hizo ni mkubwa.
Mathayo alisema watu wengi wanaoishi maeneo ya vijijini
huduma za uchunguzi wa magonjwa makubwa ikiwemo magonjwa ya moyo haziwafikii
hivyo kuwaomba wataalamu wa JKCI kufikisha huduma hizo maeneo ya mijini na
vijijini.
“Tunawaomba ikiwapendeza huduma hizi muendelee kuzitoa kwetu
hata baada ya maonesho haya, wengine hatukutarajia kama ipo siku tungepata
huduma hizi kirahisi hivi lakini bado ipo jamii ambayo inahitaji kufikiwa
msiiache”, alisema Mathayo
Katika maonesho hayo JKCI – Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato
kliniki ya moyo imeibuka mshindi wa kwanza kati ya taasisi zinazotoa huduma za
afya kutokana na umahiri na ubobezi wa wataalamu waliokuwa wakitoa huduma.
Comments
Post a Comment