Wamarekani wakutana JKCI kambi maalumu ya upasuaji wa moyo
Wataalamu wa upasuaji mkubwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Cardio Start International la
nchini Marekani wakimfanyia upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu mgonjwa
ambaye mishipa yake ya damu imeziba wakati wa kambi maalumu ya siku tano
inayofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Wataalamu wa upasuaji mkubwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Cardio Start International la
nchini Marekani wakimfanyia upasuaji wa kurekebisha mshipa mkubwa wa damu
(Aorta) mgonjwa ambaye mshipa wake mkubwa umetanuka wakati wa kambi maalumu ya
siku tano inayofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Wataalamu wa upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids
International la nchini Marekani wakimfanyia upasuaji wa kuziba tundu la moyo
wa mtoto wakati wa kambi maalumu ya siku tano inayoendelea katika Taasisi hiyo
iliyopo jijini Dar es Salaam.
Picha na: Khamis Mussa
***********************************************************************************************************
Wataalamu mabingwa wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Cardio Start International na
wengine kutoka Shirika la Mending Kids lnternatinal ya nchini Marekani wameweka
kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto na watu wazima.
Ushirikiano huo unafanywa na wataalamu hao kutokana na
uwekezaji mkubwa uliowekezwa na Serikali ikiwemo wataalamu na vifaa tiba vya
kisasa vilivyopo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mkurugenzi wa Upasuaji
wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Angela Muhozya alisema kwa
kushirikiana na shirika la Mending Kids la nchini Marekani kwa muda wa wiki
moja wanatarajia kuwafanyia upasuaji mkubwa wa moyo watoto 15 hadi 20 wenye matatizo
ya matundu kwenye moyo na wale ambao mishipa yao ya damu haiko sawa.
“Tunafanya kambi hii na wataalamu kutoka shirika la Mending
Kids kwapamoja tunashirikiana kurekebisha mishipa ya damu ambayo haijakaa
sehemu sahihi pamoja na kuziba matundu kwa watoto lengo likiwa kupunguza idadi
ya watoto wanaosubiri upasuaji wa moyo”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema kambi nyingine ya upasuaji wa moyo kwa
wiki hii ni kutoka shirika la Cardio start International la nchini Marekani
ambao wanashirikiana na JKCI kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa watu wazima wenye
matatizo ya moyo.
“Shirika la Cardio Start International wamegawanyika mara
mbili hapa tunao wataalamu wanaotoa matibabu ya kupandikiza mishipa ya damu
iliyoziba na wengine watafanya upasuaji kwa wagonjwa wa kurekebisha mshipa
mkubwa wa moyo uliotanuka au kupasuka.
“Upasuaji wa moyo kwa wagonjwa ambao mishipa yao ya damu
zaidi ya mitatu imeziba hauwezi kufanyika kwa tundu dogo, hivyo tutaufanya kwa
njia ya kufungua kifua kwa wagonjwa saba”,
“Ubobezi katika kurekebisha mshipa mkubwa wa moyo (Aorta)
uliotanuka au kupasuka unaopeleka damu shingoni, kichwani, kwenye ubongo na
katika milango ya fahamu utafanyika kwa wagonjwa watano”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema mashirikiano yote hayo yanafanyika kwa
kusudi la kuwajengea uwezo wataalamu na kuongeza ufanisi katika kutoa huduma
kwa wagonjwa wa moyo waliopo nchini.
Kwa upande wao wagonjwa wanaosubiria kufanyiwa upasuaji
katika kambi hiyo wameishukuru serikali kuwezesha upatikanaji wa matibabu ya
moyo hapa nchini.
Godfrey Mgaya kutoka Iringa ambaye mshipa wake mkubwa wa damu
umetanuka alisema amekuwa akisuribi kufanyiwa upasuaji huo ambao anaamini baada
ya kufanyiwa tatizo la kupumua alilonalo litaondoka.
“Namshukuru Mungu wiki hii nitafanyiwa upasaujia, maana
nimekuwa nikipumua kwa shida, daktari aliniambia mshipa wangu mkubwa wa damu
umetanuka na valvu moja ya moyo ahaifungi”, alisema Godfrey
Naye Francis Gurti kutoka Arusha amewashukuru wataalamu wa
afya wa JKCI na wenzao kutoka Shirika la Cardio Start International kwa
kuendesha kambi hiyo kuwasaidia wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa
moyo.
“Mimi nina tatizo la shinikizo la juu la damu lakini hivi
karibuni baada ya kupata maumivu makali upande wa ubavu wa kushoto daktari
aliniambia mshipa mkubwa wa damu umetanuka na sasa nipo hapa nasubiria
upasuaji”, alisema Francis
Comments
Post a Comment