Wananchi wafurahia huduma za matibabu ya moyo katika kliniki ya JKCI Kawe

Prince Mugisha mkazi wa Makongo akipewa maelekezo na Afisa Huduma kwa wateja wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kliniki ya Kawe Zainabu Waziri alipofika katika kliniki ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe jengo la Mkapa Health Plaza barabara ya Tuari jijini Dae es Salaam kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo.

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kliniki ya Kawe Nicholous Steven akimsikiliza Khadija Iddi mkazi wa Kigamboni aliyefika katika kliniki ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe jengo la Mkapa Health Plaza barabara ya Tuari jijini Dar es Salaam kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo.

 

Afisa Huduma kwa wateja wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kliniki ya Kawe Zainabu Waziri akimsikiliza Khadija Ally mkazi wa Mbezi chinialiyefika katika kliniki ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe jengo la Mkapa Health Plaza barabara ya Tuari jijini Dar es Salaam kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo.

****************************************************************************************************************************************************************************************************

Baadhi ya wananchi waliopata huduma za upimaji na matibabu ya moyo katika kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Kawe wilaya ya Kinondoni wameshukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasawaidia kufahamu afya za mioyo yao.

 Wakiongea kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi leo jijini Dar es Salaam wananchi hao walisema kupatikana kwa huduma hiyo kumewasaidia kufahamu afya zao na kuokoa muda kwani wamepata huduma zote ndani ya muda mfupi.

 Khadija Ally mkazi wa Kigamboni na mfanyabiashara alisema alipata  taarifa ya kuwepo kwa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo katika kliniki ya JKCI Kawe kutoka kwa mfanyabiashara mwenzake na kuamua kwenda Kawe  mapema kupata huduma hiyo.

 “Natokea kigamboni ila sikujali umbali uliopo, nilipopata tu taarifa za kuwepo kwa kambi hii niliamua kuja ili nami nipate huduma, nimefurahi sana kwani huduma niliyoipata ni nzuri . Ninaiomba JKCI itutembelee  Kigamboni na maeneo mengine nchini kutupatia huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo”, alisema Khadija.

 Naye Prince Mugisha mkazi wa Makongo juu alisema kuwepo kwa kliniki hiyo ya Kawe itawasaidia wakazi wa maeneo hayo na maeneo jirani kupata huduma na kuepuka usumbufu wa kuyafuata matibabu ya moyo makao makuu ya Taasisi hiyo iliyopo Upanga.

 “Kitendo cha  kuweka kliniki ya moyo hapa Kawe ni kizuri sana hasa kwa sisi wakazi wa maeneo jirani watakuwa wametusaidia sana na sasa tutaepuka usumbufu wa kupata huduma hii mbali na makazi yetu, sasa nitakuwa nakuja hapa mara kwa mara kuangalia mwenendo wa afya ya moyo wangu, niwapongeze tu Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa hili walilolifanya”, alisema  Prince.

 Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya JKCI Dar Group ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Tulizo Shemu alisema mwitikio ni mkubwa kwani watu wengi kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam wamefika katika kliniki hiyo kutibiwa.

 “Kiukweli mwitikio ni mzuri watu wanakuja kutoka sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam kupima afya zao na kupata matibabu,  ninawaomba  wananchi watumie nafasi hii kuja kupima afya zao kwani huduma hii ni bure kwa siku zote za kambi hii maalumu” alisema Dkt. Shemu.

 Dkt. Shemu alisema katika kambi hiyo ya siku saba ambayo imeanza jana tarehe 7 na itamalizika tarehe 13 mwezi huu wananchi watapata huduma bila malipo za kumuona daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, kufanyiwa vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na mfumo wa umeme wa moyo lakini watachangia kwa gharama nafuu huduma za maabara na dawa.

 Huduma hii inatolewa katika  kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo  Kawe jengo la Mkapa Health Plaza barabara ya Tuari kwa taarifa zaidi mwananchi anaweza kupiga simu namba 0754578190, 0783922571 na 068028000.

 Katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nchini Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefungua kliniki katika maeneo ya Kawe na Oystebay jijini Dar es Salaam pia kwa kushirikiana na hospitali mbalimbali hapa nchini inafanya kambi mbalimbali za upimaji na matibabu ya moyo lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma hizo.


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)