Wateja wa NMB Kadi za Premium kutibiwa JKCI VIP kliniki Oyster bay na Kawe
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akibadilishana mkataba wa ushirikiano wa kuwezesha
upatikanaji wa taarifa na huduma za afya kwa watoto wenye maradhi ya moyo na
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna leo wakati taasisi hizo
ziliposaini mkataba huo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna wakionesha mkataba wa ushirikiano wa kuwezesha upatikanaji wa taarifa na huduma za afya kwa watoto wenye maradhi ya moyo uliosainiwa na taasisi hizo leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa
ushirikiano na Benki ya NMB wa kuwezesha upatikanaji wa taarifa na huduma za
afya kwa watoto wenye maradhi ya moyo iliyofanyika leo katika Taasisi hiyo
iliyopo jijini Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna akizungumza
wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa ushirikiano na Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kuwezesha upatikanaji wa taarifa na huduma za afya kwa
watoto wenye maradhi ya moyo iliyofanyika leo katika taasisi hiyo iliyopo
jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi wa Benki ya NMB na wenzao wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa ushirikiano baina ya taasisi hizo kuwezesha upatikanaji wa taarifa na huduma za afya kwa watoto wenye maradhi ya moyo iliyofanyika leo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
*************************************************************************************************************
Wateja wa benki ya NMB wenye kadi za premium kutibiwa katika kliniki za VIP za Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) zilizopo Oysterbay na Kawe.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba na Benki ya NMB wa
ushirikiano wa kuwezesha upatikanaji wa taarifa na huduma za afya kwa watoto
wenye maradhi ya moyo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema
NMB imekuwa na ushirikiano mzuri wa kutoa mahitaji mbalimbali yanayohitajika
katika Taasisi pamoja na kuweka mazingira safi na salama kwa wagonjwa.
Dkt. Kisenge alisema Benki hiyo pia imeweza kutoa shilingi za
kitanzania bilioni 1 kwaajili ya kugharamia matibabu ya watoto wenye magonjwa
ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
“Mwaka 2017 NMB ilisaidia kujenga sehemu ya kukaa wagonjwa nje
(OPD) wanaotibiwa JKCI, mwaka 2022 wafanyakazi wa NMB walijitolea kuchangia
gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wanaotibiwa JKCI na mwaka 2023 Afisa
Mtendaji Mkuu wa NMB alitoa mashuka kwaajili ya wagonjwa wanaolazwa JKCI”,
alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema NMB imekuwa ikiwajali wananchi kwa
kurudisha faida wanayoipata katika jamii, na kuonesha nia ya kushiriki katika
harakati za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kusaidia pale Serikali ilipoishia nayo kukamilisha nafasi iliyobaki.
“JKCI tumeungana na NMB kuhakikisha kila mtanzania anapata
elimu kuhusu magonjwa ya moyo lengo letu likiwa kuwa na taifa lenye afya bora”,
alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth
Zaipuna ameishukuru JKCI kwa kuikaribisha Benki ya NMB kuwa mshirika mkuu
katika kutekeleza mkakati wa kutatua changamoto ya magonjwa ya moyo kwa watoto.
Ruth alisema NMB na JKCI wamesaini makubaliano yanayoenda
kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI wanaotoka
katika familia zinazoshindwa kumudu gharama za matibabu.
“NMB itatoa shilingi bilioni 1 kugharamia matibabu ya moyo
kwa watoto fedha hiyo tutaitoa kwa kipindi cha miaka minne, tunaimani mchango
huu wa shilingi bilioni 1 utakuwa msaada mkubwa hasa kwa wazazi wanaoshindwa
kumudu gharama za matibabu kwa watoto”, alisema Ruth
Ruth alisema pamoja na mchango huo Benki ya NMB itashirikiana
na JKCI kuwezesha wataalamu wa magonjwa ya moyo kutoa elimu ya magonjwa hayo
kwa wafanyakazi, wateja na wadau wengine wa NMB kuleta ufahamu wa magonjwa
hayo.
“NMB tutakuwa na wajibu wa kushiriki katika shughuli nyingine
mbalimbali za kusaidia upatikanaji wa fedha zaidi zitakazowezesha matibabu ya
watoto wenye magonjwa ya moyo hapa JKCI”, alisema Ruth
Naye mjumbe wa bodi ya JKCI Abdulmalik Mollel ameushukuru
uongozi wa Benki ya NMB kwa kuwa na wepisi wa kuchangia na kurudisha tumaini
kwa watoto wa Tanzania wanaotoka katika familia zisizokuwa na uwezo.
Mollel alisema watoto wenye magonjwa ya moyo wanazaliwa kila
siku kutokana na uumbaji wa Mungu hivyo kuitaka benki hiyo kuendelea kuchangia
matibabu ya watoto wanaohitaji mchango huo.
“Changamoto ya watoto wenye magonjwa ya moyo ipo duniani
kote, tumefarijika kuona mwanzo wako mzuri, tunaamini ushirikiano tuliouweka
hapa leo utakuwa wenye kuendelea kuleta nuru kwa watoto wetu”, alisema Mollel
Comments
Post a Comment