JKCI yafanya upasuaji wa moyo kwa njia ya mtandao



Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifanya upasuaji wa tundu dogo kwa njia ya mtandao kwakushirikiana na wenzao kutoka nchi mbalimbali duniani


****************************************************************************************************************************

Mgonjwa aliyekuwa akisumbuliwa na mishipa ya moyo na damu kuziba afanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa njia ya mtandao na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwakushirikiana na wenzao kutoka nchi mbalimbali duniani.

Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam baada ya kutoka kwenye chumba cha upasuaji wa moyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Khuzeima Khahbhai alisema wamefanikiwa  kubadilisha valve za moyo na kuzibua mishipa ya damu iliyoziba kwa kushirikiana na wataalamu kutoka sehemu mbalimbali kwa njia ya mtandao (zoom meeting).

Dkt. Khuzeima alisema kutokana na teknolojia hiyo mgonjwa anakuwa hana majeraha makubwa na baada ya siku mbili anaweza kuruhusiwa kurudi nyumbani tofauti na zamani walipokuwa wakifanya upasuaji huo kwa njia ya kufungua kifua.

“Tumefanya upasuaji wa kubadilisha valve za moyo na kuzibua mishipa ya damu  bila kufungua kifua na mgonjwa yupo salama na sasa tunategemea baada ya siku mbili ataruhusiwa kwenda nyumbani”

“Upasuaji huu unaitwa TAVr ambapo tulikuwa tukiufanya mubashara kupilia ZOOM kwa kujumuika na madatari wenzetu kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kubadilisha ujuzi na kujifunza jinsi upasuaji huu unavyofanyika”, alisema Dkt. Khuzeima.

Kwa upande wake Daktari Bigwa wa magonjwa ya moyo kutoka nchini India Dkt. Meghav Shah alisema ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania kushangazwa na uwekezaji wa vifaa vya kisasa vyenye uwezo mkubwa vilivyopo katika taasisi hiyo.

Dkt. Medhav aliongeza kuwa angependa kurudi tena Tanzania kwa mara nyingine kushirikiana na wataalamu wa JKCI na kuwaomba madaktari wengine wakipata nafasi wafike Tanzania katika taasisi hiyo kujionea namna inavyofanya kazi

“Nimeshangazwa na vifaa vya kisasa vilivyopo hapa, mitambo yao ni ya kisasa inaonyesha picha nzuri sana naona Taasisi hii ikikuwa zaidi na zaidi na kuwa moja ya kitovu kikubwa cha matibabu ya moyo Afrika”,alisema Dkt. Meghav

Naye mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huo Thomasi Sagawe alisema alikuja JKCI baada ya kupata rufaa kutoka Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) ambapo alifanyiwa vipimo na baadaye kufanyiwa upasuaji huo.

“Nilipimwa na kugundulika kuwa na shida kwenye moyo, nilipewa rufaa ya kufika JKCI ambapo nilipokelewa vizuri na kufanyiwa vipimo tena, naona sasa naendelea vizuri nawashukuru sana kwani huduma zao ni nzuri sana”, alisema Thomas

Naye Paul Sagawe mtoto wa Thomasi alisema kufanyika kwa upasuaji huo ndani ya nchi kumewasaidia sana kwani kumeokoa gharama za fedha na muda ambazo wangetumia kama wangeenda kumtibu mzazi wao nje ya nchi.

“kuwepo kwa huduma hii hapa nchini imetusaidia hatujatumia fedha nyingi ukilinganisha na ambazo tungetumia kama tungeenda kutibiwa nje ya nchi, nitumie nafasi hii kuwaambia watanzania wenzangu wakihitaji huduma za matibabu ya moyo wasihangaike kwenda nje huduma zipo hapa hapa nchini”, alisema Paul.

 


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)