Mkurugenzi wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Tulizo Waane akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi mwananchi aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre kwaajili ya
kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazofanyika katika kambi maalumu
ya matibabu inayofanyika mkoani Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpima mapigo ya moyo mwananchi aliyefika Arusha
Lutheran Medical Centre kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya
moyo zinazotolewa katika kambi maalumu ya matibabu inayofanyika mkoani Arusha.
Mfamasia wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Benito Ng’ingo akitoa elimu ya matumizi sahihi ya dawa za moyo kwa wananchi waliofika Arusha Lutheran Medical
Centre kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa
katika kambi maalumu ya matibabu inayofanyika mkoani Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpima shinikizo la juu la damu mwananchi
aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre kwaajili ya kupata huduma za upimaji
na matibabu ya moyo zinazotolewa katika kambi maalumu ya matibabu inayofanyika
mkoani Arusha.
***********************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) itahakikisha wananchi wengi wanafikiwa na huduma za kibingwa za uchunguzi
na matibabu ya moyo kupitia program yake ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hasssan.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha
na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo
inayofanyika Arusha Lutheran Medical Center.
Dkt. Peter Kisenge alisema kufanyika
kwa kambi hiyo kunatokana na kambi ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo
iliyofanyika mwezi wa sita mwaka huu jijini Arusha.
Dkt. Kisenge alisema wamerudi
tena mkoani Arusha kufanya kambi ya uchunguzi na matibabu ya moyo ili kuwapima
watu wenye matatizo ya moyo na kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo
watu 200 sawa na asilimia 30 ya watu waliojiandikisha kwa siku mbili
wamegundulika kuwa na magonjwa ya moyo.
“Kambi ya kwanza tuliyoifanya
Arusha tuliona watu 1350 tuliowakuta na matatizo ambao ni watu wazima walikuwa asilimia
14 na watoto asilimia tisa, sasa hivi asilimia imekuwa 18 ni kubwa ukilinganisha
na wakati ule hii inatokana na tunaowaona hivi sasa wengi wao ni wagonjwa na wakati
ule tuliona wasio wagonjwa na wagonjwa”.
“Vitu vinavyosababisha magonjwa
ya moyo ni pamoja na unywaji pombe kupitiliza, kutokula vyakula bora, kutokufanya
mazoezi na uvutaji wa sigara hivyo ni vizuri wananchi wafanye mazoezi ili
kupunguza kupata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo”, alisema Dkt.
Kisenge.
Alisema sababu ya pili ya kwenda
Arusha ni mkoa wa utalii wanaimarisha afya ya utalii kwa watalii, watatoa elimu
kwa wataalamu wa afya waliopo katika hospitali za Mt. Meru, Arusha Lutheran
Medical Centre na Arusha International Conference Centre (AICC) ili waweze
kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa huo.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu aliwaomba wananchi kujiunga na
bima ya afya kwa wote pindi itakapoanza kwani gharama ya matibabu ya moyo ni
kubwa lakini kama mtu akiwa na bima ya afya itampunguzia gharama ya kulipia matibabu
hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Arusha
Lutheran Medical Center Dkt. Goodwill Kivuyo aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa
kufanya kambi ya matibabu ya moyo katika hospitali hiyo ambayo imewasaidia
wananchi kupata huduma pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali
hiyo.
Dkt. Kivuyo ambaye ni
bingwa wa upasuaji aliishukuru serikali kwa kuweka mwongozo na makubaliano
ya taasisi za umma hasa za hospitali ya kuanzisha mahusiano na hospitali binafsi
jambo lililosababisha wananchi wengi zaidi kupata huduma za matibabu ya
kibingwa.
Comments
Post a Comment