Klabu ya Yanga kushirikiana na JKCI kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akisalimiana na Rais wa klabu ya Yanga Eng. Hersi Said alipomtembelea rais huyo ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona ni namna gani klabu hiyo itashirikiana na JKCI katika kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa klabu ya Yanga Eng. Hersi Said mara baada ya kumaliza mazungumzo yao ya kuona ni namna gani klabu hiyo itashirikiana na JKCI katika kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo, kutoa uelewa kwa jamii kuhusu magonjwa ya moyo na kutangaza huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Rais wa klabu ya Yanga Eng. Hersi Said na wafanyakazi wa JKCI wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mazungumzo ya kuona namna ambavyo klabu hiyo itashirikiana na JKCI katika kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo,kutoa uelewa kwa jamii kuhusu magonjwa ya moyo na kutangaza huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo.
***********************************************************************************************************************************************************************************************************************
Klabu ya mpira ya Yanga imeahidi kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo, kutoa uelewa kwa jamii kuhusu magonjwa ya moyo na kutangaza huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Rais wa klabu ya
Yanga Eng. Hersi Said wakati akizungumza na viongozi wa JKCI walipomtembelea
ofisini kwake kwaajili ya kuona ni namna gani klabu hiyo itashirikiana na JKCI.
Eng. Hersi alisema katika ushirikiano huo wataanza kwa kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto kwa kushiriki
chakula cha jioni chenye lengo la
kuchangisha fedha hizo za matibabu kilichoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete tarehe 2 Novemba mwaka huu
katika Hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.
“Taasisi hii imekuwa ikitoa huduma kwa jamii tunahitaji kuwa
na ushirikiano nayo kwa muda mrefu kwa
asilimia 100, sisi tutaanza kwa
kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto wasiokuwa na uwezo kwani tuna ndugu zetu ambao
ni wagonjwa wa moyo na sisi pia tunaweza kuumwa hivyo basi ni muhimu kuisaidia
jamii yenye uhitaji”.
“Pia tutatangaza huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa,
tutawapeka wachezaji wetu kupima afya za mioyo yao kwani wanawataalamu
waliobobea katika matibabu ya moyo pia wanavifaa vya kisasa vya kupima na
kutibu moyo”, alisema Eng. Hersi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema asilimia 70 ya gharama za matibabu ya
moyo kwa watoto wanaotibiwa katika taasisi hiyo yanalipwa na Serikali na
asilimia 30 iliyobaki inalipwa na JKCI pamoja na wadau mbalimbali.
“Katika Taasisi yetu kuna watoto 1500 wanasubiri kufanyiwa
upasuaji wa moyo na asilimia kubwa wanatoka katika familia zenye uchumi mdogo
hivyo basi ninawaomba wadau mbalimbali waweze kushirikiana nasi katika kuchangia matibabu ya watoto hawa kwani tatizo ni kubwa na
tunahitaji kuwasaidia ili wapate huduma”,.
“Ninaishukuru klabu ya Yanga kwa kukubali kushirikana nasi katika chakula cha jioni kwa kuchangia gharama za matibabu ya watoto kwani
kuna watoto ambao wanatakiwa kufanyiwa upasuaji wa haraka hii ni ndani ya mwezi
mmoja baada ya kuzaliwa na kuna wengine wanaweza kusubiri baada ya muda fulani
ndipo wakafanyiwa”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake mjumbe wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Abdulmalick Mollel aliishukuru klabu ya Yanga kwa kuamua kushirikiana na JKCI
katika kuchangia matibabu ya watoto wasio na uwezo na kutoa elimu kwa jamii
kuhusu magonjwa ya moyo.
“Magonjwa ya moyo ni moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza na yanaweza kuepukika kama wananchi watafuata ushauri wa kitaalamu hii ikiwa ni pamoja na kuwa na uelewa wa jinsi ya kujikinga na magonjwa haya, ninaamini tukishirikiana kwa pamoja watu wengi watakuwa na uelewa wa kutosha wa magonjwa haya na kuepukana nayo”, alisema Mollel.
Comments
Post a Comment