Watu 604 wachunguzwa na kutibiwa moyo Arusha
Baadhi ya wananchi waliofika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) wakisubiri kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa ALMC. Watu 604 walipata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo 83 kati yao wakiwemo watoto 21 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.
Mfamasia wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Benito Ng’ingo akitoa elimu ya matumizi sahihi ya dawa za moyo kwa wananchi waliofika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika mwishoni mwa wiki mkoani Arusha.
****************************************************************************************************************************************************************************************************
Jumla ya watu 604 wamepata huduma za uchunguzi na
matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha Lutheran Medical Centre
(ALMC).
Akizungumza kuhusu kambi hiyo ya siku tano iliyomalizika
mwishoni mwa wiki Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge alisema asilimia kubwa ya watu waliowaona walikuwa na tatizo
la shinikizo la juu a damu.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo na mishipa
ya damu alisema kuna wagonjwa ambao waliwakuta na shida ya mfumo wa umeme wa
moyo, misuli ya moyo kushindwa kufanya kazi
na kwa upande wa watoto waliwakuta na matatizo ya valvu na matundu.
“Katika kambi hii watu wote 604 tuliowaona tuliwafanyia
vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa umeme wa moyo na
vipimo vya maabara. Wagonjwa 83 wakiwemo
watoto 21 tuliwakuta na matatizo ya moyo yaliyohitaji uchunguzi na matibabu
zaidi hivyo basi tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”.
“Tumetoa elimu ya kufuata mtindo bora wa maisha ambao
utawasaidia watu kutokupata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo hii ikiwa
ni pamoja na kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kutokutumia bidhaa aina ya
tumbaku na kutokunywa pombe kupitiliza pia tumetoa elimu ya matumizi sahihi ya
dawa”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema licha ya kutoa huduma za upimaji na matibabu
kwa wananchi lakini pia wamewajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hiyo
ambao kwa sasa wanaweza kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema miundombinu iliyopo Arusha
Lutheran Medical Centre (ALMC) iko vizuri na yote iko katika kuboresha afya ya
watanzania na wananchi wa Arusha.
“Kambi hii ya matibabu hapa ALMC itakuwa endelevu, siku ya jumatatu
(leo) madaktari wetu bingwa bobezi watakuwepo hapa wakitoa huduma kwa wananchi, ninawaomba wananchi mje kupima afya za mioyo
yenu mapema kwa kufanya hivi kwa wale watakaokutwa
wagonjwa kutawapunguza madhara katika mioyo yao na kuepukana na gharama kubwa
za matibabu”, alisema Dkt. Waane.
Dkt. Waane ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo na mishipa ya
damu alisema kliniki ya matibabu ya moyo itakuwepo kila siku ALMC na wananchi
watapimwa vipimo vyote vya moyo pamoja na kupewa dawa kwa wale watakaogundulika
kuwa na shida na watakaokutwa na matatizo makubwa zaidi watapewa rufaa ya
kwenda kutibiwa JKCI.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Arusha Lutheran Medical Centre
(ALMC) Dkt. Godwill Kivuyo aliishukuru Serikali
kwa kuwatuma wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwenda
ufanya kambi ya upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Arusha
katika hospitali hiyo.
“Kambi hii ya matibabu imefanyika kwa muda wa siku tano na uitikio umekuwa mkubwa kwani watu wengi wanashida wanahitaji kupata huduma za matibabu ya moyo, ninawashukuru JKCI kwa kuliona hilo na kuamua kuwa na kliniki endelevu ya matibabu ya moyo hapa ALMC”, alisema Dkt. Kivuyo.
Comments
Post a Comment