JKCI na ALMC kutoa huduma bobezi za matibabu ya moyo Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda akimjulia hali mwananchi aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali hiyo. Kushoto ni Mhudumu wa afya wa Arusha Lutheran Medical Centre Damas Marko.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda akiangalia eneo la mapokezi la Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) alipotembelea hospitali hiyo leo kwaajili ya kuangalia huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wananchi na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali hiyo. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ALMC Dkt. Godwill Kivuyo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda akimsikiliza Mkurugenzi wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alipotembelea Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwaajili ya kuangalia huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wananchi. Katikati ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimweleza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda jinsi chumba cha huduma ya dharura cha Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kilivyokuwa katika kiwango cha kimataifa wakati mkuu wa mkoa huyo alipetembelea hospitali hiyo leo kwaajili ya kuangalia huduma za kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wananchi.
***********************************************************************************************************************************************************************************************
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwakushirikiana na hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) wameanza safari ya pamoja ya utoaji huduma bobezi za magonjwa ya moyo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo watalii na watu mbalimbali wanaotembelea Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hayo yamesemwa Jijini hapa na Mkurugenzi wa JKCI Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kambi maalum waliyoifanya ambapo zaidi ya ya wagonjwa 500 wameonwa ikiwemo watoto 40 pamoja na rufaa kwa wagonjwa zaidi ya 60 watakaotibiwa JKCI akiwemo mtoto Witness Julius(10) aliyegundulika kupata shida kweye valvu za moyo.
Alisema JKCI imeanza safari ya utoaji huduma za magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na ALMC kama tawi bobezi la utoaji wa huduma hizo na muda si mrefu wataanza kufunga mitambo maalumu ya matibabu hayo yatakayowezesha watanzania na wanaafrika mashariki kupunguza gharama za kuzifuata Jijini Dar es Salaam na kutumia gharama nyingi.
"Mtoto Witness ataondoka kwa kutumia gari langu kama Mkurugenzi kwaajali ya kwenda JKCI kuanza matibabu kwani ameacha shule akiwa darasa la nne kutokana na kuumwa lakini alikuwa na shida ya valvu na kutibiwa kama mgonjwa wa kawaida na hapa tutafunga mitambo ya kisasa na nje ya nchi na wanaEAC watakuja hapa A LMC kwaajili ya kupata huduma za kibobezi za moyo", alisema Dkt. Kisenge.
Alisema vifaa vilivyopo ALMC vinakidhi viwango vya ubora lakini pia watalii watakuwa na amani sababu ya hospitali ya JKCI, ALMC na hospitali ya Rufaa ya Mount Meru lazima mkoa wa Arusha uwe Kituo cha utalii tiba kwa Kanda ya Kaskazini
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ALMC, Dkt. Godwill Kivuyo alishukuru ushirikiano huo na kuongeza kuwa hospitali hiyo itaendelea kutoa huduma mbalimbali za kibobezi katika magonjwa ya moyo na mengine kwa kushirikiana na hospitali nyingine kwani hivi sasa wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha ushirikiano huo kwaajili ya kuhakikikisha wananchi na wanaafrika mashariki wanapopata huduma bora za afya.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda alisema ALMC imeanza kazi rasmi za kutoa huduma za kibobezi chini ya usimamizi wa JKCI ikiwemo ongezeko la huduma nyinginezo kwani Arusha iwe ni kitovu cha nchi za EAC katika kuhakikisha huduma bora za matibabu zinakua kwa kasi na kutoa rai Kwa wananchi kutokunywa dawa bila kujua wanaumwa ugonjwa gani hivyo ni vema wafike hospitali na kupima ili kubaini aina ya magonjwa na kupata dawa husika zinazotibu ugonjwa uliobainika.
RC Makonda alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, akitaka hospitali zote kuwa na huduma za kibingwa ili kutoa urahisi wa wananchi kupata matibabu hayo katika maeneo ya karibu bila kusafiri umbali mrefu.
"Tunataka Arusha iwe na hospitali ya kibingwa itakayosaidia jamii na watu kutoka mataifa mbalimbalimbali kupata huduma za afya na pia uwe ni mkoa mfano katika huduma hizi bobezi", alisema Mhe. Makonda.
Wakati huo huo, Kaimu Katibu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Solomon Sangweti alishukuru ushirikiano huo utakaowezesha hospitali ya ALMC kuwa ya kwanza ndani ya EAC katika utoaji wa huduma za afya huku Abdulmalik Mollel ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii Tiba aliongeza kuwa uwepo wa hospitali hiyo utawezesha Mkoa wa Arusha kupata zaidi katika utoaji wa matibabu ya kibobezi ndani na nje ya nchi za EAC.
Comments
Post a Comment