Wafanyakazi wa JKCI watakiwa kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wa serikali za mitaa
Afisa Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Vida Mushi akitoa ripoti ya tathimini ya mwaka wa pili wa utekelezaji wa mpango mkakati wa JKCI kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye akitoa maoni yake wakati wa kikao
cha kupokea ripoti ya tathimini ya mwaka wa pili wa utekelezaji wa mpango
mkakati wa taasisi hiyo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Ghati Chacha akiwakumbusha wafanyakazi wa taasisi hiyo kujaza
taarifa zao za kazi wanazozifanya kila siku katika mfumo wa kupima utendaji wa
kazi za watumishi wa umma (PEPMIS) wakati wa kikao cha kupokea ripoti ya
tathimini ya mwaka wa pili wa utekelezaji wa mpango mkakati wa JKCI kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Paul Josephat akiuliza swali a wakati wa kikao cha kupokea
ripoti ya tathimini ya mwaka wa pili wa utekelezaji wa mpango mkakati wa JKCI kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia ripoti ya tathimini ya mwaka wa pili wa utekelezaji wa mpango mkakati wa JKCI wakati ikisomwa na Afisa Mipango wa JKCI Vida Mushi kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
***********************************************************************************************************************************************************************************************
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wa serikali za mitaa ili waweze kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Angela Muhozya wakati akiongeza na
wafanyakazi hao katika kikao cha kupokea ripoti ya tathimini ya mwaka wa pili wa utekelezaji
wa mpango mkakati wa taasisi hiyo.
Dkt. Angela alisema ni muhimu kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo
wakazitumia tarehe 11-20 za mwezi huu kwaajili ya kujiandikisha katika daftari hilo
ili ifikapo tarehe 27 mwezi Novemba wawe na sifa za kupiga kura na kuwachagua
viongozi wa serikali za mitaa.
“Tunaelekea katika
uchaguzi wa serikali za mitaa ambao
umebeba maendeleo ya nchi yetu na yetu binafsi kwa siku za mbeleni, ninawaomba kila
mtu katika eneo analoishi aende kujiandikisha ili wakati wa uchaguzi ukifika
mkachague viongozi wazuri watakaoshirikiana na wananchi kutuletea maendeleo ya
taifa letu”, alisisitiza Dkt. Angela.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa mpango mkakati huo Dkt.
Angela ambaye ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi aliwapongeza
wafanyakazi hao kwa kujitoa kwao kufanya kazi kwa bidii na kujituma na kuwataka
kuongeza jitihada zaidi katika kutoa huduma kwa wananchi.
“Mpango mkakati wetu unaisha mwaka 2025/26 huku ukiwa na maadili ya
msingi ya ushirikiano, uadilifu, weledi na ubunifu ninaamini kila mmoja wetu
akiyatekeleza haya tutatimiza malengo
yetu ya kutoa huduma za moyo zenye uthibitisho, mafunzo na utafiti”, alisema
Dkt. Angela.
Akiwasilisha ripoti ya tathimini ya mwaka wa pili wa utekelezaji
wa mpango mkakati wa taasisi hiyo Afisa Mipango wa JKCI Vida Mushi alisema walipima kwa
kuangalia malengo waliyojiwekea yamefanikiwa kwa kiasi gani, uelewa wa
wafanyakazi katika mpango mkakati huo na changamoto zilizopo katika utekelezaji.
“Baada ya kuangalia vipimo tulivyojiwekea tuligundua mpango
mkakati wetu kwa mwaka 2024 umefanikiwa kwa asilimia 80 ukilinganisha na mwaka
jana ulifanikiwa kwa asilimia 73, ninaamini tukifanya jitihada zaidi tutafikia
asilimia 100 katika utekelezaji”.
“Ninawaomba wafanyakazi wenzangu tufanye kazi zetu kwa kufuata malengo ya taasisi ili kuiwezesha
taasisi yetu kufika dira yake ya kuwa taasisi inayotambulika kimataifa katika
kutoa huduma, mafunzo na kufanya utafiti wa magonjwa ya moyo”, alisema Vida.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati Chacha aliwakumbusha wafanyakazi
hao kujaza taarifa zao za kazi wanazozifanya kila siku katika mfumo wa kupima
utendaji kazi za watumisi wa umma (PEPMIS) kwa wakati kuliko kusubiri wakati
mwaka wa fedha unaisha.
“Majukumu yenu ya kazi mnazozifanya kila siku yako katika mpango mkakati wa taasisi ni muhimu kila wiki mkajaza kazi mlizozifanya kwa wiki husika kwa kufanya hivyo kutawasaidia kupata alama nzuri za utendaji wa kazi na kuepukana na mzigo wa kujaza kazi za mwaka mzima mwishoni wa mwaka wa fedha”, alisema Ghati.
Comments
Post a Comment