Dkt. Kisenge: Uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe ni hatari kwa mjamzito
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpa zawadi mwananchi aliyefika katika
Taasisi hiyo kwaajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ikiwa ni muendelezo
wa kuadhimisha siku ya moyo duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 29
Septemba.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu akimkabidhi zawadi ya chakula mama wa mtoto aliyelazwa katika hospitali hiyo ikiwa ni muendelezo wa kuadhisha siku ya moyo duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 29 Septemba.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu akiwakabidhi chakula ndugu wa mgonjwa aliyelazwa katika hospitali hiyo ikiwa ni muendelezo wa kuadhisha siku ya moyo duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 29 Septemba.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Nuru Letara akimpa zawadi mzazi wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo ikiwa ni muendelezo wa kuadhimisha siku ya moyo duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 29 Septemba.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI) Mainda Hamu akimpa zawadi mzazi wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo ikiwa ni muendelezo wa kuadhimisha siku ya moyo duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 29 Septemba.
****************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Na Anna Nkinda - JKCI
Wajawazito wametakiwa kula vyakula bora na kuacha
uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kipindi cha ujauzito ili waweze kujifungua
watoto wenye afya bora .
Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akigawa zawadi kwa watoto wenye
matatizo ya moyo wanaotibiwa katika taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es salaam.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema moja ya sababu zinazopelekea mtoto kuzaliwa na magonjwa ya moyo ni uvutaji
wa sigara na unywaji wa pombe kipindi cha ujauzito.
“Ni vyema kina mama wajawazito wakajikinga na magonjwa ya
moyo na kuepuka kufanya vitu ambavyo vitapelekea kuzaa mtoto mwenye matatizo ya
moyo hii ikiwa ni pamoja na kuacha kuvuta sigara na kunywa pombe”,.
“Nawasihi wazazi
kuleni vyakula bora ikiwa ni pamoja na mboga za majani na matunda, fanyeni mazoezi ili kupunguza uzito mkubwa kwani uzito mkubwa
unaweza kukupelekea kujifungua mtoto mwenye kisukari na ugonjwa huu unaweza kusababisha mtoto kupata magonjwa ya moyo” ,
alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
na Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Sulende Kubhoja alisema
kumekuwa na dhana katika jamii kuhusu magonjwa ya moyo ni kwa watu wazima tu
lakini siyo kweli kwani magonjwa hayo yanawapata hata watoto wadogo.
“Jamii inatakiwa kufahamu kuwa hata watoto wadogo wanaumwa
magonjwa ya moyo ila kwa upande wao mara nyingi huwa ni magonjwa ya kuzaliwa
nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio
wake lakini pia kuna ambao wanayapata ukubwani na huwa ni matatizo ya valvu”.
“Tangu maadhimisho ya siku ya moyo yalipoanza mara nyingi watu huwatazama watu wazima na
kusahau watoto wadogo, ndio maana tumeona kama taasisi tutoe zawadi kwa watoto
na kuwarudishia tabasamu. Ninaiomba jamii siku kama ya leo kukumbuka watu wote
iwe ni kwa mtoto ambaye hajazaliwa au aliyezaliwa mwenye ugonjwa wa moyo na
yule mkubwa wote ni sawa inatupasa kuwakumbuka”, alisema Dkt. Kubhoja.
Naye Mainda Hamu ambaye ni Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alisema
wao kama wauguzi wamekuwa wakikaa muda mwingi na watoto wodini wamepata faraja
kuona watoto wamepata zawadi ambazo zimewafanya watabasamu pia wazazi wao
wamefurahi kupata mahitaji ya muhimu ya kila siku ambayo yatawasaidia wakiwa
hospitali.
“Watoto na wazazi wao wamefurahi siku hii ya leo imekuwa
faraja kwao kwani kuwapatia watoto zawadi za kuchezea na mahitaji yao ya muhimu
ya kila siku wakati wa kuadhimisha siku ya moyo duniani ni jambo jema
linaloleta upendo na faraja kwa wagonjwa”, alisema Mainda.
Akizungumza kwa niaba ya wazazi wenzake Zuhura Mkamba mama mzazi
wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo katika taasisi hiyo aliwashukuru
wafanyakazi wa JKCI kwa kuwapa zawadi na
kusema kuwa wamepata faraja kuona madaktari na wahudumu wengine wa afya
wanajitoa na kuwapa zawadi wao na watoto
wao.
“Licha ya wafanyakazi wa hospitali hii kutuhudumia katika
matibabu lakini pia wametupatia zawadi jambo hili ni la kibinadamu sana ninawaomba
watu wengine waige mfano na kuwakumbuka wagonjwa waliopo mahospitalini ili
kuwapa faraja”.
Comments
Post a Comment